Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, mwenye barakoa akitoa uamuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya Serikali ya Kijiji cha Wita na Kanisa la AICT Bujora uliodumu kwa miaka kadhaa.Kulia wa kwanza ni Diwani wa Kisesa (CCM), Marko Kabadi.Picha zote na Baltazar Mashaka.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza kwenye eneo la mgogoro uliohusisha Kanisa a AICT na Serikali ya Kijiji cha Wita, Kisesa.Kulia nyuma ya Mkuu huyo wa Wilaya ni Katibu Mkuu Kiongozi wa AICT, Mchungaji Josephales Mtebe, aliyevaa suti(kushoto), ni Mzee wa Kanisa la AICT Bujora, Mathias Ndeto.
**********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Magu
MKUU wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli,jana amechukua uamuzi mgumu kutatua mgogoro wa ardhi kati ya Serikali ya Kijiji cha Wita,Kata ya Kisesa na Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Bujora, uliodumu kwa miaka kadhaa.
Eneo hilo lililokuwa likigombewa kati ya serikali ya kijiji na taasisi hiyo ya dini,Kanisa la AICT lilidai lilimilikishwa na serikali ya kijiji mwaka 1987,likaliendeleza kwa kujenga shule ya sekondari Bujora ambapo jiwe la msingi liliwekwa na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Kalli alisema baadhi ya mambo na migogoro yanahitaji busara kuitatua na yawezekana kwenye mgogoro huo anatafutwa mchawi,hivyo watashirikiana wote kuutatua na kutoa fursa kwa pande mbili kwenye mgogoro huo wakiwemo wadau wengine ili kuupatia ufumbuzi,kabla ya kuelekea kwenye eneo la tukio.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Wita, Michael John Migeto, alisema mwaka 2018 alikuwa mjumbe wa serikali ya kijiji, hawakuwahi kutoa ardhi hiyo kwa kanisa bali waliihodhi wakati wakijenga uzio wa shule kwenye eneo halali walilolipata kutoka kwa wananchi waliokuwa wakilimiliki kwa kuwalipa fidia.
“Madai kuwa eneo hilo ni mali ya kanisa, ushahidi ni mihtasari ya kijiji na nyaraka za kuthibitisha umiliki wa ardhi hiyo, hawana,”alisema Migeto.
Mzee wa Kanisa la AICT Bujora, Mathias Ndeto, alisema hoja ya kuendeleza ardhi hiyo kama taasisi wasingeweza wakati wameomba kupimiwa, hivyo kinachoonekana kuna maslahi ya watu wachache wanaolihitaji eneo hilo.
“Hoja ya kutoendeleza eneo, utawezaje wakati umeomba kupimiwa, pia unaendelezaje bila umiliki ? Wataalam wa ardhi hawatajatenda haki,wangelipima mgororo usingekuwepo,lakini tangu mwaka 1987 leo wananchi ndio wanaibua mgogoro kudai eneo ni lao, wakuliwa wapi?” alihoji.
Mmoja wa wananchi,Cosmas Nyalali alisema kanisa halina vielelezo vya kujitosheleza zaidi ya eneo walilojenga uzio,waliombwa mihutasari ya kijiji iliyowamilikisha, nayo hawana.
Alidai mgogoro huo uliibuka mwaka 2019 baada ya kijiji kutaka kujenga soko ambapo aliwatuhumu maofisa ardhi kupokea fedha bila kuzingatia sheria kuwa chanzo cha mgogoro, kwamba eneo hilo ni mali ya kijiji, kanisani halikuwahi kuuziwa.
Katibu Mwenezi wa CCM, Wilaya ya Magu, Nyeoja Mkangara,kabla ya mgawanyo wa vijiji eneo hilo lilikuwa la wazi,si la mtu wala taasisi, lakini baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji iliyopita walijigawia na kujenga nyumba za makazi.
“Kanisa haliwezi kutoa rushwa ila kwa ubora na utamu wa eneo maana tunakwenda kuwa wilaya,wanaweza kuandika barua za upenyo kupata haki hiyo lakini mgogoro huu chanzo ni watumishi wa serikali,”alisema.
Katibu Mkuu Kiongozi wa AICT,Mchungaji Josephales Mtebe,alisema hawana tatizo na wananchi wa Wita na baada ya kubaini tatizo walikutana viongozi na wanavyo vielelezo vya umiliki wa ardhi hiyo,vinginevyo isingekuwa rahisi kupanda miti na kuchimba kisima.
Alisema wananchi kwa kutambua eneo hilo ni la kanisa,ndio maana serikali ya kijiji iliwapa miezi 6 kuliendeleza na kwamba mgogoro huo uliibuliwa mwaka 2019 kwa maslahi ya watu.
Diwani wa Kisesa (CCM) Marko Kabadi, alisema si muumini wa kupiga kelele zaidi ya demokrasia,waliotengeneza mgogoro huo na kuukuza ni serikali yenyewe tangu mwaka 1987 na kuonya hilo liwe fundisho na waliohusika wanapaswa kutubu.
Akihitimisha mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Magu,alisema “eneo linalodaiwa ni mali ya serikali ya kijiji kuna miti na kisima, kwa mamlaka aliyopewa eneo hili libaki kwa kanisa waliendeleze, kama kuna shida ambao hawataridhika waende mahakamani.”
Mchungaji Mtebe baada ya uamuzi huo,aliishukuru serikali kwa kuwa mgogoro huo ulikuwa uonevu kwa kanisa ambalo linatafuta na kuhimiza amani huku akieleza kuwa walifuata taratibu kwenye kadhia hiyo kabla ya kuibuka mwaka 2019.
Aidha aliiomba serikali ya wilaya, mkurugenzi mtendaji wa wilaya wajeree ombi la ili wapimiwe eneo hilo na kupewa hati waliendeleze kisheria kwani wana mipango ya kujenga chuo cha sayansi za tiba afya tawi la Kolandoto.
Awali Mtendaji wa Kijiji cha Wita,Mashimba June, alisoma barua ya Kanisa hilo la AICT Bujora mwaka Januri 4,2021 kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu wakiomba kupimiwa eneo hilo ili waandaliwe hati ya umiliki waliendeze na kuhudumia jamii.
Pia ilieleza mgogoro huo Januari 29, 2020 uliwahi kushughulikiwa na Dk. Philemon Sengati ambaye kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu na kuelekeza uongozi wa kanisa kumwandikia barua mkurugenzi mtendaji wa wilaya.