Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa serikali kwenye ukumbi wa mikutano wa IOM Kibondo mkoani Kigoma Septemba 18, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu,
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa watumishi wa Serikali wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Mikutano wa IOM Kibondo Septemba 18, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu ili waweze kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali za kimaendeleo na hawapaswi kuwa wala rushwa.
Pia amewataka watumishi hao wahakikishe wanafanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa pamoja na kusimamia vizuri fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 18, 2021) wakati akizungumza na watumishi wa umma wilayani Kibondo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii mkoani Kigoma.
Amesema kuwa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajia kuona mipango yote ya Serikali inatekelezwa katika jamii kwani kufanya kazi kwa bidii kutasaidia wananchi kujishughulisha na mambo mengine ya maendeleo.
“Wito wa Rais Mheshimiwa Samia ni kuona uchumi unaenda kwa kasi kuanzia mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla, tulianza na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuwawezesha watanzania kufanya shughuli zao za kiuchumi”
Waziri Mkuu amewataka watumishi hao kuwahamasisha na kuwawezesha Watanzania kujishughulisha shughuli za kiuchumi. “Kama ni mkulima alime sana, kwenye migodi wafanye kazi sana, wanafanyabiashara wafanye sana biashara hata wanaosoma wasome sana”
Amesema watumishi washiriki kikamilfu katika kusimamia makusanyo ili kuwawezesha kutekeleza miradi wanayoiona italeta tija kwa wananchi. “Kigezo cha ukusanyaji wa mapato kipimwe kutokana na ujenzi wa miradi ambayo inawahudumia wananchi.”
Waziri Mkuu pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wahakikishe kuwa miradi yote inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha iliyotolewa “Wakurugenzi simamieni utekelezaji wa miradi katika maeneo yenu ili Wakuu wa Wilaya wakija kuizindua ionekane thamani ya mradi huo”.