******************************
Na Dorina G. Makaya – Kagera, Rusumo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeelezea kuridhishwa kwake na hatua mbalimbali za ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo MW 80 unaotekelezwa kwa kuzingatia makubaliano ya Kiserikali ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo kila nchi itapata MW 27.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Seif Gulamali, kufuatia ziara ya kamati hiyo kwenye mradi huo tarehe 12 Septemba, 2021.
Amesema, tumejionea na kuridhika na hatua mbalimbali za ujenzi zilizofikiwa, lakini pia tumeona kuna fursa za ajira kwa watanzania na kwa nchi za Rwanda na Burundi.
Makamu mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, amewaomba wadau wa maeneo ya Ngara, waweze kuulinda mradi huo wa kimkakati.
“Mradi ni wa kwetu, unapoharibika mradi huu maana yake tunajiumiza sisi wenyewe kama watanzania. Kwa hiyo tuulinde mradi huu. Alisema Gulamali.
Makamu Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, zaidi ya asilimia 75 ya mradi umejengwa katika ardhi ya Tanzania kwa hiyo ni kama mradi ni wa Tanzania hivyo uchukuliwe kwa uzito wake.
Akizungumzia kuhusu baadhi ya mapungufu yaliyobainika, Gulamali ameitaka TANESCO kulifanyia kazi suala zima la malipo ya fidia, kuyahakiki ili usitumike mwanya wa fedha za fidia kulipwa wasiostahili.
Ameweka bayana kuwa, kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeelekeza kuwa, fidia ilipwe kwa watu waliohakikiwa, na baada ya kujiridhisha wanaostahili walipwe haki zao. Aidha, ametahadharisha kuhusu tabia ya kuibuka kwa wadai fidia wengine wanaojitokeza baada ya wahusika kulipwa fidia.
Gulamali ameiomba Serikali ya mkoa wa Kagera na Wilaya ya Ngara wasimamie kwa umakini sana mradi wa umeme wa Rusumo ikiwa ni pamoja na kuulinda kuepuka wavamizi kwenye eneo la mradi.
Akizungumzia kuhusu ukosefu wa zimamoto panapotokea majanga ya moto, Gulamali ameiomba wizara na serikali kwa ujumla Kuhakikisha gari na vifaa vya zimamoto vinapatikana na kuwepo katika eneo la mradi ili kuulinda mradi na maisha ya watu.
Awali, mbunge wa jimbo la Ngara Ndaisaba Ruhoro, aliieleza kamati ya bunge kuhusu malalamiko ya wananchi wa wilaya ya Ngara kutokulipwa fidia zao na pia kuhusu ukosefu wa zimamoto katika eneo la mradi.
Akizungumza wakati wa majumuisho, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewahakikishia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa Wizara ya Nishati itasimamia usiku na mchana ili kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo MW 80 unakamilika kwa wakati ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Amesema, kukamilika kwa mradi huo, kutatatua kero ya tatizo la umeme na kuhakikisha kuna upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu katika mkoa wa Kagera na kuimarisha upatikanaji wa umeme mkoani Kigoma na Katavi
Mradi wa umeme wa Rusumo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 340 sawa na takriban shilingi bilioni 816, mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya dunia (WB) na utakapokamilika utazalisha MW 80 na kila nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi zitapata MW 27 kufuatia makubaliano ya kiserikali yaliyoingiwa mwaka 2012.