Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Songea na Namtumbo(Sonamcu Ltd) mkoani Ruvuma Juma Mwanga kulia akiwasikiliza jana baadhi ya wakulima wa zao la Tumbaku wa kijiji cha Suruti wilayani Namtumbo waliolalamikia juu ya tozo ya asilimia mbili iliyokatwa katika zao hilo.
Picha zote na Muhidin Amri
………………………………………………………………….
Na Muhidin Amri,Namtumbo
WAKULIMA wa zao la Tumbaku katika wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma,wamelalamikia makato ya asilimia 2 yaliyofanywa na Serikali kupitia
Mamlaka ya mapato Nchini (TRA) katika msimu wa kilimo 2021.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao jana, wakulima wa Tumbaku kutoka Chama
cha Msingi cha Suruti(Suruti Amcos) wameshangazwa na hatua ya Serikali
kuwakata fedha kwa kila kilo moja ya tumbaku bila kuwashirikisha wakulima
ambao ndiyo wanaotumia nguvu na gharama kubwa katika uzalishaji.
Shami Ponera amesema,tozo ya asilimia mbili kwa kila mkulima sio sahihi
kwani Serikali tayari imeshakata kodi yake kupitia Chama Kikuu cha
Ushirika cha Namtumbo na Songea(Sonamcu).
Amesema, hatua hiyo ni sawa na uonevu mkubwa kutokana na unyonge wao,kwani
haiwezekani hata kidogo wakulima wakatwe tozo mara mbili na kuiomba
Serikali iangalie suala hilo upya kwani linawaumiza sana wakulima.
Kwa mujibu wa Ponera,zao la Tumbaku ni gumu katika uzalishaji wake kwa kuwa
linachukua takribani miezi tisa tangu hatua ya awali hadi linapofikiswa
sokoni, kwa hiyo ni vizuri Serikali ikaangalia upya juu ya tozo hiyo
ambayo inawakandamiza na kuwarudisha nyuma wakulima wa zao la Tumbaku.
Ameiomba Serikali, kuhakikisha inarudisha fedha ilizochukua kwa wakulima
ili ziweze kuwasaidia kujiandaa na msimu mpya wa kilimo kwa kuwa ni haki
yao ya msingi, na Serikali haijatoa msaada wowote kwa wakulima wakati wa
maandalizi ya zao hilo.
Mkulima mwingine Ali Chemka amesema, suala la tozo ya asilimia mbili kwa
mkulima wa Tumbaku halikufanyika kwa haki kwani serikali ilitakuwa
kuwataarifa kwanza kwakulima kabla haijaanza kukata tozo hiyo ili kuona
uhalali wake.
Chemka ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika(Sonamcu
Ltd)amesema, tozo hiyo imeleta mgogoro mkubwa kati ya wakulima na uongozi
wa Sonamcu na kuiomba Serikali itumie hekima na busara na kurudisha fedha
ilizochukua kwa wakulima.
“mimi sikatai kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,hata hivyo
ninachoomba ni muhimu sana kuwepo na mawasiliano kati ya mlipa
kodi(mkulima) na serikali badala ya maamuzi hayo kufanywa na upande
mmoja”amesema Ponera.
Amesema,wakulima wa Tumbaku wanakabiliwa na changamoto nyingi katika
uzalishaji wa Tumbaku, kwa hiyo ni vyema serikali iangalie upya suala hilo
ambalo kimsingi linawarudisha nyuma wakulima.
Chemka amesema, baadhi ya wakulima wana madeni makubwa ya fedha
walizochukua kutoka katika taasisi za fedha na kwa watu binafsi ambazo
wanategemea kulipa baada ya kuuza Tumbaku kwa hiyo hatua ya Serikali ya
kukata fedha kina hatarisha maisha na usalama wa wakulima.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Sonamcu Juma Mwanga amesema,kodi ambayo
Serikali imewatoza wakulima katika msimu wa kilimo 2020/2021 imekuja ghafla
na Serikali haikustahili kukata kodi ya asilimia mbili kwa wakulima.
Mwanga amesema, kisheria tozo hiyo inatakiwa kukatwa pale wakulima
wanapouza Tumbaku kwa makampuni na watu binafsi siyo wanapouza kwa Chama
cha Ushirika.
Mwanga ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo kupitia upya sheria hiyo
hususani kwa zao la Tumbaku ambalo uzalishaji wake unakabiliwa na
changamoto kubwa na ni vyema kodi hizo zielekezwe kwenye mazao mengine
badala ya Tumbaku.
Ameshangazwa na hatua ya Serikali kuwakata wakulima asilimia mbili,
wakati Sonamcu kama chama cha wakulima wa Tumbaku imeshalipa Dola za
Marekani zipatazo 13 sawa na Sh. Milioni 32.
Amesema,ni makosa kuwakata tozo wakulima wanaouza Tumbaku yao kwa vyama vya
Ushirika kwani sheria ya kodi ya mwaka 2021 inataka mkulima kulipa kodi
pale atakapouza Tumbaku kwa makampuni au watu binfasi na sio kwa vyama vya
msingi na vyama vikuu vya ushirika.
Aidha ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo na wizara ya fedha, kukaa
na kutafsiri upya sheria hiyo kama vyama vya msingi na vyama vya ushirika
vinastahili kukatwa tozo hiyo.
Amesema wakulima hawakatai kulipa kodi, lakini Serikali ilitakiwa kukaa na
wadau ili kujadili na kutoa elimu kabla haijaanza kukata kodi hiyo ili
kupata maoni.
Kwa mujibu wa Mwanga ni kwamba, kama itaendelea kushikilia msimamo wa
kukata tozo kwa wakulima basi kuna uwezekano mkubwa wa kushuka kwa
uzalishaji wa Tumbaku katika msimu wa kilimo 2021/2022.