Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Elias Masalla anatarajiwa kuzindua kikundi cha mchezo wa mbio za kawaida (Jogging Club) na mazoezi ya viungo kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili na kujenga uhusiano mzuri baina ya wananchi zitakazofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Sabasaba siku ya Jumamosi ya Septemba 11, 2021 kuanzia saa kumi na mbili asubuhi.
Hayo yamebainishwa na afisa tarafa wa wilaya ya Ilemela Ndugu Godfrey Mzava wakati akiwasilisha taarifa fupi ya maandalizi ya uzinduzi wa klabu hiyo ambapo amesema kuwa lengo la kuanzisha klabu hiyo ya mbio ni kutekeleza agizo la Rais Mhe Samia Suluhu Hassan la kutaka wananchi kufanya mazoezi kwaajili ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuifanya kama njia ya kujikinga ugonjwa wa UVIKO-19
‘… Kama mnakumbuka Mhe Rais Samia alishawahi kuelekeza wananchi kufanya mazoezi, Sisi tumeamua kutekeleza agizo hili kwa vitendo lakini pia hii inaweza kuwa kama njia ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 …’ Alisema
Aidha Ndugu Mzava akawaomba wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kwaajili ya kushiriki mbio hizo sambamba na kuendelea kushirikiana na Serikali yao katika kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Ndugu Kizito Bahati Sosho mbali na kuwaomba wadau kuunga mkono jitihada za uanzishwaji wa klabu hiyo ameongeza kuwa mbio hizo zitakuwa endelevu na kwa siku hiyo ya uzinduzi wake litafanyika pia zoezi la hiari la uchangiaji damu, upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza na utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO-19