Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia gazeti la RAI MWEMA kwa muda wa siku thelathini (30) kutokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari .
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dodoma Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari Mhe.Gerson Msigwa amesema gazeti hilo limekiuka masharti ya leseni liliyopewa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni mwa jamii na vilevile kuwafanya wananchi waichukie Serikali na viongozi wake.
“Mifano michache ya habari na makala ambazo kwa kiasi kikubwa zilikiuka masharti ya leseni, misingi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ni pamoja na gazeti toleo Na.844 la tarehe 21 Agosti, 2021 lililochapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Maumivu mapya 17”. Katika habari hii gazeti lilikwenda kinyume na vifungu vya 52(1) (a), (c), (d) na (e) pamoja na 54(1) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 kwa kuchapisha na kusambaza habari zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na wananchi kwa kuonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawaletea maumivu wananchi kwa kuweka tozo 17 za kazi mbalimbali za wasanii”. Amesema Mhe.Msigwa.
Aidha amesema gazeti la Raia Mwema toleo Na.853 ukurasa wa 1 na kuendelea ukurasa wa 3 na wa 4 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “Hamza wa CCM hatari,”. Kwanza kwa kuonekana dhahiri kukosa weledi na udanganyifu gazeti hilo lililotolewa tarehe 3 Septemba, 2021 liliandikwa limetolewa tarehe 3 Agosti, 2021 na katika habari hiyo linawanukuu watu wawili lililowaita Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Manumba, mara linamtaja DCI Wambura.
“Gazeti hili lilitaka kuuaminisha umma kuwa Hamza ni mwanachama wa CCM ama kiongozi wa CCM (Chama Tawala) bila kuwa na uthibitisho usioacha shaka yoyote, jambo ambalo linaweza kuleta chuki miongoni mwa wanachama wa CCM na makundi mengine ya jamii huku likijua kuwa kuandika habari hiyo ni kinyume na kifungu cha 50(1) (b),(d), (e) na kifungu cha 52(1) (e) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016”. Amesema
Pamoja na hayo amesema katika gazeti hilo hilo toleo Na. 853 ukurasa wa 1 na kuendelea ukurasa wa 3 liliandika habari yenye kichwa kisemacho ‘DC kizimbani akidaiwa Milioni 100’. Habari hii ilikosa weledi na maadili ya uandishi wa habari kwani kichwa cha habari hiyo hakikushabihiana na maudhui yaliyoandikwa katika habari hiyo kwa kuonesha kuwa DC anayezungumzwa yupo madarakani wakati mwandishi alijua kuwa anamzungumzia DC ambaye tayari alikuwa ameshastaafu.
Amesema Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari inaamini kuwa adhabu hii itawapa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa Uandishi wa Habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya habari.
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa wahusika hawataridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari, wanayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari ndani ya siku thelathini (30) tangu siku ya uamuzi huu.