TATIZO la uhaba wa walimu wenye utaalamu wa lugha ya alama, ukosefu wa miundombinu rafiki na zana duni za kujifunzia na kufundishia katika baadhi ya shule za msingi mkoani Singida kumetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kwa watoto wenye mahitaji maalum katika kupata elimu ya awali.
Hayo yalibainishwa na wanafunzi wenye mahitaji maalum; wakiwemo wasioona na wenye ualbino, wanaosoma shule ya Msingi Mchanganyiko Mgori, halmashauri ya Wilaya ya Singida wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya lugha ya alama Septemba 23 mwaka huu.
Walisema kuwa licha ya Serikali kutekeleza Sera ya elimu jumuishi inayotaka wanafunzi wenye mahitaji maalum kusoma na wenzao katika shule moja bila kubaguliwa, suala la uhaba wa walimu wa lugha ya alama, vifaa maalum vya kujifunzia, kufundishia na miundombinu duni bado ni kikwazo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Amiri Mohamed alisema kuwa shuleni hapo hakuna vifaa muhimu vya kujifunzia kwa wenye ulemavu kama vile Mashine na vitabu vyenye maandishi ya nukta nundu na karatasi maalum kwa ajili ya kuchorea, hali inayosababisha wasioona kutegemea hisani au msaada wa wenzao wanaoona kuwasomea maandishi ya kawaida ubaoni ndipo waweze kuandika kwenye vibao vyao.
“Mtihani unaletwa kwa maandishi ya kawaida kwa wote, sisi wenye mahitaji maalum na wenzetu wanaoona, sasa sisi mpaka mwenzio akusomee…..yaani ni mateso kuliko unavyoweza kudhani na hapo hakuna mwalimu wa lugha ya alama ambaye anaweza kukusaidia” alisema Amiri.
“Hapa hakuna bweni. Tunakolala ni chumba ambacho awali lilikuwa darasa kabla ya kukarabatiwa kuwa Ofisi ya walimu na sasa ndilo ‘bweni’ letu” alisema Obed Williard, mwanafunzi mwingine na kuongeza;
Mimi hapa angalau nina uoni hafifu lakini wapo wenzangu ambao hawaoni kabisa. Tunaishi kwenye hili ‘bweni’ ambalo vyoo vyake ni vya nje. Hebu fikiria changamoto zinazowakumba wasioona….Wanaweza kuumwa na wadudu wenye sumu kali, nyoka au hata kudhuriwa na watu wabaya”
Mwalimu wa kitengo cha Elimu Maalum katika shule hiyo, Hemed Kilango alikiri kukabiliwa na changamoto kubwa katika kuwafundisha watoto hao kwani hakuna zana muhimu na bajeti yao ni ndogo kiasi kwamba haitoshi kununulia hata kofia, miwani ya jua au mafuta ya ngozi kwa wanafunzi wenye ualbino.
Ofisa elimu maalum katika Wilaya ya Singida, Huruma Funda alisema kuwa halmashauri hiyo inahitaji jumla ya walimu 20 wa elimu maalum wakati waliopo ni sita tu, wawili kati yao ni wa lugha ya alama.
Aidha, alisema kuwa zipo shule za msingi Jumuishi 31 katika halmashauri hiyo ambazo hazina walimu wa elimu maalum hali inayosababisha walimu wa kawaida katika shule hizo kutoa elimu kwawanafunzi hao.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Action Aid katika shule 20 za wilaya ya Singida na Chamwino Dodoma unaonesha asilimia 0.5 (Singida) na asilimia 0.34 (Chamwino) ya watoto wote walioandikishwa shule mwaka 2018 walikuwa wenye ulemavu wakati Kitaifa watoto 49,625 wa aina hiyo waliandikishwa ikiwa ni sawa na asilimia 0.5 ya watoto wote walioandikishwa shule kipindi hicho.