Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika toka wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo leo (03.09.2021) ambapo ameonya vitendo vya watendaji hao kulalamika badala yake watafute suluhisho la kero za wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati) akiongoza kikao cha viongozi wa vyama vya ushirika ambapo amewataka kuhakikisha wanabuni mikakati ya kuwezesha wakulima kupata masoko na pembejeo kwa kutumia mfumo wa ushirika.
Mrajis Msaidizi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika toka Makao Makuu Dodoma, Bw. Robert George akizungumza kwenye kikao na viongozi wa vyama vya ushirika wa mkoa wa Rukwa leo Sumbawanga ambapo amewataka wawe na utaratibu wa kuepuka madeni yenye kuumiza wanachama.
Wawakilishi wa viongozi wa vyama vya ushirika toka wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (hayupo pichani) leo mjini Sumbawanga kilichohusu kujadili kero za ushirika na kutafuta ufumbuzi wake
******************************
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti amewataka viongozi wa vyama vya ushirika wa wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kuacha tabia ya kulalamika badala yake wahamasishe ushirika unaolenga kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Mkirikiti ametoa agizo hilo leo (03.09.2021) mjini Sumbawanga alipokutana na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa cha Rukwa (UCU) pamoja na wanachama wake 60 kujadili changamoto za madeni na ushirika kutokidhi malengo ya wanachama.
“Ushirika li alia hauna nafasi kwenye mkoa wa Rukwa kwani Serikali ya Awamu ya Sita inataka kuona wanaushirika wakinufaika na vyama vyao , hivyo Viongozi achene tabia ya kulalamika bali tafuteni majawabu ya kero za wakulima na wafugaji” alisema Mkirikiti.
Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa Ushirika una historia iliyotukuka kwani kupitia ushirika watoto wa masikini walipata elimu na kuchangia maendeleo ya taifa na familia zao dhidi ya umasikini hivyo uwepo wa chama kikuu cha uShirika Ufipa uwe ni suluhisho la kuleta maendeleo kwa wana Rukwa siyo migogoro na madeni.
“Wakati mkulima wa Rukwa analalamika kupanda kwa gharama za pembejeo na kukosa masoko ya mazao hapo ndipo Viongozi wa vyama vya ushirika wanapotakiwa kubuni suluhisho na kuwasaidia wananchama wao “ alisisitiza Mkirikiti.
Katika hatua nyingine Mkirikiti amesema uwepo wa Chama kikuu cha Ushirika Ufipa (UCU) usaidie wakulima ,wavuvi na wafugaji kupata pembejeo ,masoko pia mitaji ili wanachama wapate faida na kukuza uchumi wao.
Kuhusu tatizo ukosefu wa soko la mahindi na mazao mengine Mkirikiti amesema viongozi wa ushirika wanalo jukumu la kutafuta taarifa za masoko kila siku na kuwafikishia wanachama wao.
Akijibu ombi la Chama kikuu cha ushirika kuhusu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuongeza kiwango cha tani za ununuzi mahindi ,Mkirikiti alisema haitoweza kununua mahindi yote kutokana na kusudi la serikali.
“NFRA ni taasisi ya kimkakati ya kuhakikisha taifa linakuwa na usalama wa chakula ,hivyo haiwezi kununua mahindi yote ya wakulima” alisema Mkirikiti.
Akizungumza kuhusu utendaji kazi wa Chama Kikuu cha Ushirika Ufipa Rukwa ( UCU) Mwenyekiti wake Adabeth Mbuyani alisema changamoto kubwa inayokabili ushirika ni ukosefu wa masoko na gharama kubwa za pembejeo .
Akizungumza kwa niaba ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika toka Makao Makuu ,Mrajis Msaidizi Robert George alisema wamefika Rukwa ili kushiriki kikao hicho na kutambua changamoto za wananushirikikufuatia uwepo wa malalamiko mengi.
Robert aliongeza kusema uhai wa chama cha ushirika unatokana na uwepo wa mitaji hatua itakayosaidia chama kuwa na uwezo wa kutoa huduma ikiwemo pembejeo na masoko ya mazao.
“Nguvu ya ushirika inatokana na wanachama wenye hisa za kutosha ndio maana tunahamasisha vyama kuwa na mitaji hatua itakayosaidia kuwa na nguvu za kiuchumi kuweza kutoa huduma kwa wadau wake “ alihitimisha Mrajis Msaidizi huyo kutoka Dodoma.
Kikao hicho ni cha kwanza cha Mkuu wa Mkoa huyo chenye lengo la kufufua uhai wa vyama vya ushirika ambapo kimehudhuriwa na taasisi za fedha za NMB, CRDB, TADB, Eliagro, HELVETAS pamoja na Maafisa ushirika wa wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.
Mwisho.
Imeandaliwa na ;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa,
SUMBAWANGA
03.09.2021