Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani akifungua leo mafunzo kwa Viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo.
Baadhi ya Viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani Tabora wakiwa katika mafunzo ya kuwajengea uwezo leo.
Picha na Tiganya Vincent
****************************
NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka Viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika kujaza fomu za maadili ili kuongeza uwajibikaji na uwazi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa umma.
Alisema hatua hiyo itasaidia kusimamia na kuendesha shughuli za vyama vya ushirika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Masharti ya Vyama vya Ushirika kwa kudhibiti vitendo vya wizi, ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwao.
Balozi Dkt.Batilda alitoa kauli hiyo leo wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo.
Alisema viongozi baada ya kujaza fomu watakakwenda kinyume watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za Nchi na zile zinaongoza ushirika ili kuepuka kuegeuza ushirika chaka la wanyang’anyi wa mali za wanyonge.
Mrajis Msaidizi Mkoa wa Tabora Absalom Cheliga alisema kwa Viongozi wapya wa Vyama Vikuu vya Ushirika baada ya mafunzo ya siku tatu watajaza fomu za maadili na kujaza za tamko la mali.
Alisema utaratibu wa kuwataka viongozi wa vyama vya ushirika kujaza fomu za maadili na kutoa matamko ya mali ambazo wanamilimiki ulikuweko lakini ulikuwa hatutekelezwi na hivi sasa wameamua kuutekeleza ili kuongeza uwazi kwa wanachama wanaowaongoza.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Tabora amewaagiza viongozi wapya wa Ushirika kuhakikisha wanaondoa kasoro zinazotokana na mfumo wa upandaji miti na malipo yake kwa kuja na mfumo mbadala ambao utakuwa na tija kutokana na makato ya fedha.
Alisema fedha wanazotozwa wakulima wa tumbaku kwa ajili ya zoezi la upandaji miti lazima zitafutie mfumo mpya wa kutekeleza zoezi hilo ili uwe na tija kwa ulinzi wa mazingira na uendelevu wa mistu asili.
Alisema wakulima wa tumbaku wamekuwa wakikatwa fedha kwa ajili ya kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kufidia pengo la miti wanayotumia katika ukaushaji wa tumbaku lakini utekelezaji wake umekuwa sio wa kuridhisha.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka viongozi wapya kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa Tumbaku kwenye vyama vya msingi vya Ushirika kwa kuwachukulia hatua wale wote wataohusika.
Aliongeza wakati wa utumishi wao wahakikshe wanasimamia vizuri mikopo inayotolewa kwenye kilimo cha Tumbaku na kujiepusha na kutokujihusisha na rushwa ya aina yoyote katika Sekta ndogo ya zao la Tumbaku.
Aliongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa mpana viongozi hao ili waweze kusimamia majukumu ndani ya vyama vyao na kuondoa kero zilizokuwa zinawakabili wanachama wao.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba Ushirika una malengo makubwa katika kumletea maendeleo mwananchi kupitoa kilimo cha mazao mkakati yaliyowekewa kipaumbele Tumbaku na Pamba.
Aliwataka viongozi hao kuwa na mahusiano mazuri na wadau kwani ndiyo njia pekee ya ya kuondokana na migongano ndani ya vyama vyao.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanawahusisha viongozi wa vyama vikuu vya Igembensabo, Wectu na Milambo vyote vya mkoani Tabora.