…………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
ASKARI 72 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye vituo mbalimbali vya Viwanja vya Ndege nchini wamepandishwa vyeo vya ukoplo baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya uongozi yaliyofanyika kwenye Chuo cha Jeshi hilo cha Chogo kilichopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Wazimamoto waliotunukiwa vyeo hivyo ni kutoka Viwanja vya ndege vya Mwanza, Dodoma, Lindi, Mpanda, Kigoma, Kilwa Masoko, Moshi, Arusha, Manyara, Mtwara, Masasi, Musoma, Shinyanga, Songea, Tabora, Tanga, Songwe na Julius Nyerere JNIA).
Hata hivyo, wazimamoto hao ni miongoni mwa Wazimamoto 400 wa jeshi hilo waliopata mafunzo hayo kwa nchi nzima, ambapo wengine wapo kwenye vituo vingine tofauti na viwanja vya ndege.
Akitunuku vyeo hivyo leo kwa Wazimamoto wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi hilo, ambaye pia ni Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji kwenye Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), SACF Elia Kakwembe amewataka wahitimu hao kuendelea kufanya vyema kwa kujituma zaidi kwenye majukumu yao na sio kubweteka baada ya kupewa cheo hicho. maana bado wapo chini ya uangalizi.
“Sasa msiende kutambia baa hivi vyeo mjue cheo ni dhamana, tunataka muendelee kufanya vizuri maana nyie mmeshakuwa viongozi na mtakuwa mnafuatiliwa kwani cheo sio kabila wala jina la mtu na ukifanya ndivyo sivyo kinaondolewa mara moja na tutaendelea kuwafuatilia,” amesema Afande Kakwembe.
Hatahivyo, amewataka Wazimamoto hao kuwa wabunifu kwa kuibua mambo mazuri ya kuifanya JNIA kusonga mbele zaidi katika masuala ya uzimajimoto na uokoaji.
Naye Kaimu Kamanda wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha JNIA, Mkaguzi Maria Luoga amewataka wahitimu hao kuzingatia ‘U 10’, ambazo ni uzalendo ambapo askari anatakiwa kuwa mzalendo kwa nchi, jeshi na kituo chake cha kazi, pia awe na upendo baina ya wenzake na raia, hali kadhalika awe na uvumilivu hususan katika nyakati za hatari.
“U nyingine ni pamoja na askari lazima awe na uhakika na umakini wa kila jambo analofanya, pia awe na uelewa na ukakamavu, pia wawe watanashati katika mavazi yao na mwisho wawe na utii kwa kila mtu ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi,” amesema MRFFS Luoga.