Naibu waziri wa fedha na mipango ,Hamad Masauni wakiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa chuo Cha uhasibu Arusha( IAA) wakati alipotembelea chuo hicho kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa chuoni hapo (Happy Lazaro)
Aliyeko kushoto ni Mkuu wa chuo Cha uhasibu Arusha,Profesa Eliamani Sedoyeka akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa fedha na mipango Hamad Masauni wakati alipotembelea chuo hicho kujionea miradi mbalimbali inayoendelea chuoni hapo (Happy Lazaro)
***************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Yussuf Masauni, amevitaka vyuo nchini kutoa elimu inayoendana na uhitaji wa soko la ajira kwa kuwaandaa vijana kuweza kujiendeleza wenyewe .
Ameyasema hayo wakati alipotembelea chuo cha uhasibu Arusha (IAA) na kukagua majengo matatu yatakayokuwa na maktaba ya vitabu, mabweni na sehemu ya chakula.
Masauni amesema kuwa ,ni vizuri vyuo vikajikita katika kutoa elimu ambayo itawezesha kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto ya ajira huku wakiwaondolea dhana ya kusubiri kuajiriwa badala yake wajiandae kujiajiri.
“nje ya vijana kuandaliwa kujiajiri pia ni vizuri wakajikita katika kutumia taaluma yao kufanya tafiti mbalimbali zitakazoisaidia Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwani vijana kama hawa tunawategemea Sana katika jamii.”amesema.
Aidha Masauni amekipongeza chuo hicho kwa ujenzi wa jengo la chakula litakalogharimu zaidi ya Sh 1.3 bilioni ambalo linatarajia kukamilika Oktoba mwaka huu.
Aidha jengo lingine alilotembelea ni pamoja na kituo cha ukuzaji na uendelezaji wa biashara na kitengo cha Tehama ambayo yapo katika hatua nzuri ya ujenzi.
“kwa kweli baada ya kutembelea miradi hii nimeridhishwa na kuona miradi ya serikali iliyoanzishwa kwa fedha za ndani ipo katika hatua nzuri na zinajengwa katika viwango vilivyotakiwa na maeneo ambayo mtahitaji msaada wetu kama Serikali sisi tutakuwa tayari kuwasaidia.”amesema Masauni.
Ameongeza kuwa,miradi hii muhimu kwa wanafunzi wetu kama ujenzi wa mabweni ya wanafunzi hususani wa kike kwani yatasaidia Sana kwa usalama wao kwa kukaa mazingira ya chuo lakini kwa chuo watapata kipato cha pango watakazolipa na kujiletea maendeleo ya chuo”alisema.
Aidha amesema kuwa, serikali iko tayari kuongeza nguvu kwa yale maeneo ambayo watahitaji msaada ili kuongeza kasi ya kuwaandaa wanafunzi kuwa tayari kwa ajili ya maisha yao na wahitimu wanaomaliza fani mbalimbali chuoni waweze kujiajiri na kujiendeleza wenyewe, badala ya kusubiri kuajiriwa.
Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kwa sasa chuo kinatekeleza miradi mitatu ikiwemo jengo la darasa, ofisi, na bweni ambavyo vyote vitagharimu kiasi cha shs 15 bilioni.
Profesa amesema kuwa,wanatarajia Oktoba mwaka huu wanafunzi wataongezeka kutokana na chuo kuongeza baadhi ya fani lakini pia uboreshaji huo wanaoufanya .
Prof.Sedoyeka amesema kuwa, ujenzi wa bweni unoendelea chuoni hapo, kwa awamu ya kwanza unakadiriwa kubeba wanafunzi 2000 huku matarajio ni kufikisha wanafunzi 5000 ifikapo mwakani.
“Tunaalika wenye nyumba karibu na chuo chetu ambao wanania ya kugeuza majengo yao mabweni, tutayakagua na tukijiridhisha tutawaweka wanafunzi wetu huko” ameongeza.
Amesema katika upande wa kitengo Cha ubunifu kwa wanafunzi, ni mpango endelevu na wanafunzi wote watalazimika kuja na wazo la kibiashara ili kuwaandaa wataalamu bobezi watakaoendana na soko la ajira.
Aidha amefafanua kuwa,wamekuwa wakiwaunganisha wanafunzi wao na makampuni ya umma pamoja na binafsi na mabenki na kuweza kupata uzoefu pamoja na ajira kulingana na uhitaji waliona.