****************************
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
DIWANI wa Kata ya Mbwewe Halmashauri ya Chalinze ,Mkoa wa Pwani Omary Msonde, amewaagiza walimu Sekondari Changarikwa kuacha tabia ya kuwarudisha wanafunzi nyumbani wanaodaiwa pesa ya chakula, badala yake wazazi wawajibishwe.
Aidha amewaonya wazazi na walezi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwalipa fedha za chakula, akisema kwamba watawaita kwenye kikao maalumu kuzungumzia suala hilo.
Msonde ametoa agizo hilo baada ya kurudishwa shuleni hapo wanafunzi walioondolewa kwa kukosa pesa za chakula, ambapo alisema awali wanafunzi wanaodaiwa pesa hizo walirudishwa nyumbani kabla ya kurejea shule kuendelea na masomo yao, huku akiwataka ambao hawajaripoti wafanye hivyo mapema.
“Tumewarejesha shule watoto asilimia 80 ya waliorudishwa nyumbani kwa kukosa pesa za chakula, uamuzi huo uliochukuliwa na uongozi wa shule haukuwa sahihi kwani mwanafunzi hausiki na utafutaji wa pesa, jukumu lake ni kusoma hivyo kumfukuza shule ni kumwonea,” alisema Msonde.
Alieleza kuwa alipopata taarifa za kufukuzwa kwa wanafunzi hao alikutana na uongozi wa shule, na Kata wakazungumzia suala hilo, tayari agizo hilo limeshatekelezwa ambapo wanafunzi asilimia 80 wamesharejea shuleni, huku akiagiza waliosalia waripoti haraka.
“Sanjali na hilo pia nimeagiza uongozi wa shule uwasiliane na wazazi wa wanafunzi ambao bado hawajaripoti wafike shule maramoja, pia waandae kikao na wazazi au walezi wa wanafunzi ambao wanadaiwa pesa za chakula wazungumzie suala hilo,” alisema Msonde.
Aidha ameshangazwa kuwepo kwa madeni hayo kwa wanafunzi husika pasipokuitwa wazazi wao kuzungumzia, mpaka kufikia kiwango kikubwa hali ambayo kwa namna moja au nyingine inamrudisha nyuma kimasomo mwanafunzi husika.
“Nimewaambia walimu na ofisa elimu kwamba ni marufuku kuwarudisha nyumbani wanafunzia wanaodaiwa pesa ya chakula, badala yake wazazi waitwe ikiwezekana wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na si kumfukuza mwanafunzi,” alisema Diwani huyo.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Asha Sizya amemshukuru diwani huyo, huku akielezea masikitiko yake kutokana na mtoto wake kukaa nyumba kwa wiki mbili kwa sababu ya yeye kukosa pesa ya chakula.