NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,mkoani Pwani ,Sara Msafiri ametoa siku tano kwa wafanyabiashara ndogondogo wa Soko la Picha ya Ndege ,waliogoma kuondoka katika eneo la hifadhi ya barabara ili kumpisha mkandarasi aendelee na ujenzi wa barabara kuu .
Akizungumza na wafanyabiashara hao,wakati wa ziara ya kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ), Kibaha Mjini ,Msafiri alieleza amesikia wapo vinara na baadhi ya wafanyabishara wanadaiwa kuchochea kushinikiza wafanyabiashara wengine wasihame katika eneo lililotengwa.
Msafiri alisema wafanyabiashara walitakiwa kuhamia , eneo la shirika la elimu ambalo lipo river road Msufini lakini wamekaidi na kudai kuwa hakuna wateja na wengine wamekosa vizimba.
“Hili eneo ni hatarishi na Tanroad walishawaelekeza mhame ili mkandarasi aendelee na ujenzi ,mnatakiwa mhame pia kwa usalama wa maisha yenu kujilinda na ajali “
Msafiri ameeleza ifikie hatua jamii ikaacha kuingiza masuala ya siasa katika maendeleo .
Nae mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini ,Maulid Bundala alisisitiza wafanyabiashara waliogoma kuondoka.
Bundala alisema ,katika masuala ya kijamii na maendeleo watu waache kuingiza siasa na uchama hali inayokwamisha juhudi za serikali .
Awali mmoja wa wafanyabishara hao ,Anelista Mbaga alibainisha mgogoro huo ni wa muda mrefu,mwanzo walitakiwa kuhamia eneo la Lulanzi ambako waliona ni mbali , baadae wakatakiwa kuhamia eneo la River road ambako wachache wamegomea .
Mbaga alieleza ,yeye na baadhi wametii kuhama lakini hawapati wateja kwani wote wanaishia kwa wafanyabiashara wa barabarani.