***********************************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Kamati ya siasa mkoa wa Njombe imefanya ukaguzi na kuridhishwa na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa mkoani humo na kuupongeza uongozi wa wilaya kwa kusimamia vyema miradi hiyo.
Kamati hiyo iliongozwa na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala sambamba na kamati ya siasa wilayani humo pamoja na viongozi wa serikali ambapo ilitembelea miradi minne ambayo ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Figanga iliyopo kata ya Madope, ujenzi wa maabara shule ya sekondari Mavala kata ya Milo, ujenzi wa maabara shule ya sekondari Ikovo kata ya Ludende pamoja na ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mdilidili kata ya Lugarawa.
Akizungumza katika ziara hiyo mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala amewapongeza viongozi wa wilaya hiyo kwa kutekeleza vyema ilani ya chama cha mapinduzi kwani wanapokamilisha vyema miradi ya ujenzi wanakuwa wametimiza matakwa ya serikali ya chama cha mapinduzi.
Ameongeza kuwa si kwamba hakuna mapungufu kabisa isipokuwa mapungufu yaliyopo ni madogo madogo ambapo yameonekana katika baadhi ya miradi hiyo ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho.
“Hakuna kizuri kisichokosa kasoro, hii miradi mmeitekeleza kwa ubora mzuri na katika kiwango kinachotakiwa isipokuwa kuna kasoro ndogo ndogo kama marekebisho ya ubao wa kuandikia shule ya msingi Figanga, sakafu katika maabara ya Mavala na vinginevyo”, Alisema Mwamwala.
Aidha kwa upande wa katibu wa CCM mkoa wa Njombe Amina Imbo amewataka viongozi wa serikali pamoja na kamati ya siasa ya wilaya kujenga mazoea ya kutembelea miradi mara kwa mara ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kiwango kinachotakiwa badala ya kutembelea jengo likiwa lumekamilika kitu ambacho kitawalazimu kubomoa na kujenga upya.
Amesema ukaguzi wa mapema huepusha hasara ambayo inaweza kujitokeza na kuokoa muda kwani muda utakaotumika kubomoa na kujenga upya ingekuwa ni muda wa kutumia majengo.
Sunday Deogratias ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizoonekana ili kuweza kuyafanya majengo hayo kuwa bora zaidi.
Miradi hiyo imetekelezwa kwa nguvu za wananchi na serikali ambapo katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Figanga vimejengwa kwa shilingi milioni 44 ambapo wananchi wamechangia shilingi milioni 15 na zilizobaki ambazo ni milion 29 zimechangiwa na serikali, ujenzi wa maabara shule ya sekondari Mavala imegharimu shilingi ml. 58 wananchi wamechangia milioni 28 laki moja na elfu sita, ujenzi wa zahanati ya Mdilidili imetumia jumla ya ml. 79.4 pamoja na vifaa tiba nguvu ya wananchi milioni 46 laki nane na arobaini, mfuko wa jimbo milioni 12 laki 7 na telathini.