**********************************
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima ametoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya dawa asilia na umuhimu wa chanjo kwa watu ili kuongeza kinga za miili yao.
Dkt. Gwajima amesema hayo leo akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na shughuli za Maendeleo ya Jamii Mkoani Mara.
Dkt. Gwajima amesema kuwa, pamoja na juhudi za kuelimisha umma kuhusu UVIKO-19 zinazoendelea, baadhi ya watu wasio waaminifu wanarudisha nyuma jitihada zinazofanywa na Serikali katika mapambano ili kuutokimeza ugonjwa huo.
Amesema matumizi ya tiba asili sambamba na huduma za chanjo inayoendelea kote nchini ni sehemu ya afua zinazohitaji elimu endelevu ili kuwezesha jamii kujikinga dhidi ya janga la UVIKO 19 linalousumbua ulimwengu.
“Hata darasani kwenye mtihani haiwezekani wanafunzi kupata A kwa pamoja ipo asilimia kama 30 ya wanafunzi watapata asilimia kubwa, darasa litaendelea kupata weingine asilimia 20, asilimia 20…asilimia nyingine inayobaki hata ukifanya nini, watabakia hivyo hadi tuition, hivyo hata suala la UVIKO 19, liko hivyo elimu lazima iwe endelevu” alisema.
Aliendelea kusema kuwa, tangu kuanza kwa UVIKO mwezi Januari, 2020 kuna mambo mengi yamejitokeza kuna baadhi ya watu kwa makusudi wanapotosha ukweli, kwa lengo la kuchafua hali ya hewa na kuharibu heshima na hadhi ya hayati aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati JPM.
“Kwanza mwaka jana wakati UVIKO unaingia nchini chanjo haikuepo, … mtakumbuka hayati akiwa Chato alisema tutumie dawa asili kujifunza kama njia ya kujinusuru… nami nilitoa maelekezo kama Waziri wa Afya,…tiba ya asili ipo na ilikuwepo, inaendelea kutumika,” alisema na kuongeza kuwa baada ya chanjo ya UVIKO 19 Serikali imejiridhisha na usalama wake hivyo kushauri wananchi kuanzia miaka 18 wajitokeze kuchanja ili kuongeza kiwango cha kinga ya mwili dhidi ya maradhi hayo.
Alifafanua kuwa, baadhi ya nchi ugonjwa wa UVIKO-19 umeanza kuwapata watoto na baadaye hali inaweza kuwa mbaya zaidi, hivyo kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuwasikiliza Wataalamu wa Afya kwa kupata chanjo ili kuzinusuru afya zao.
“Ubishi huu ukiendelea na kupotosha umma, tutakuwa tumawaonea watoto kwa sababu kirusi kitakuwa kinaendelea kuogelea na kuhatarisha maisha ya watoto” tuendelee kuchukua hatua kwa kuchanja ili tujikinge sisi na Watoto wetu vinginevyo tutaishia kwenye kifo.
Hata hivyo ameendelea kutoa rai kwa wananchi kutumia mitandao vizuri ili kupata taarifa sahihi za njia za sayansi ya kujikinga dhidi ya UVIKO-19 ikiwemo njia ya kuchoma chanjo, badala ya kutumia mitandao kupotosha wananchi kwa manufaa yao binafsi.
” Fuatilia kisayansi kuhusu elimu ya COVID, …Tumia simu kuhama kisayansi kuhusu maambukizi ya waliochanjwa na wasiochanjwa. Badala ya kutumia simu kwa WhatsApp na mitandao ya kijamii pekee”
Ameongeza kwa kusema kuwa, Serikali itaendelea kutoa Elimu kwa wananchi na kutoa fafanuzi zote kuhusu umuhimu wa kutumia afua ya chanjo katika kujikinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ili kulinda Afya za Watanzania wote.
“Amesema baadhi ya viongozi wa Dini wanapotosha umma…lakini baadhi ya vitabu vinaeleza kuwa watu wangu wanakufa kwa kukosa maarifa…. lazima tutafakari na kufuatilia kwa karibu umuhimu wa chanjo na matokeo ya maambukizi kwa waliochanjwa na wasiochanjwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Mara kwa Waziri wa Afya, Katibu Tawala wa Mkoa Albert Msovela amesema Mkoa huo ni unakabiliwa na upungufu wa watumishi, vifaa tiba na madaktari Bingwa hivyo kumuomba Waziri kuukumbuka Mkoa wa Mara kwenye ajira za Watumishi ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Juma Mfanga amesema hadi tarehe 16/08/2021 Mkoa umechanja watu 4,856, na kusisitiza kuwa kama Mkoa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajitokeze zaidi kupata chanjo ili kujikinga wao na familia zao dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Aidha, amesema Mkoa unakabiliwa na uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa na hivyo kupunguza ufanisi wa utendaji katika Mkoa wa Mara.