Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Mkutano kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Songwe.
……………………………………………………………………………
Na Lydia Churi- Mahakama, Songwe
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa wadau wa Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika kazi zao ili kuendana na Mahakama ya Tanzania ambayo imeshaanza matumizi hayo na ifikapo mwaka 2025 kazi zake zote zitakuwa zikifanywa kwa mtandao.
Akizungumza na wadau wanaofanya kazi na Mahakama wakati akihitimisha ziara ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Songwe, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania haiwezi kuwa ya mtandao kama wadau wake hawataingia kwenye matumizi hayo kwa kuwa mnyororo wa upatikanaji wa haki unawahusisha wadau wote.
“Ukiiangalia ramani ya Mkoa wa Songwe utagundua kuwa kwa jinsi ilivyo, wananchi wengine wa mkoa huo watalazimika kufuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu hivyo Tehama ndiyo jibu”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza wadau hao kuwekeza kwenye Tehama.
Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya Tehama ambapo uwekezaji huo ukitumiwa vizuri utauwezesha Mhimili huo kulingana na Mahakama nyingine duniani zenye maendeleo makubwa katika matumizi ya Tehama ifikapo mwaka 2025.
“Mahakama tumefanya uwekezaji mkubwa katika Teknolojia, ili tufikie Mapinduzi ya nne ya viwanda tutasukumwa na matumizi ya Tehama”, alisema Jaji Mkuu.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili za mkoa wilaya za mkoa wa Songwe, Jaji Mkuu aliwataka wajumbe hao kusimamia Maadili na nidhamu ya Mahakimu kwa kuwa wajumbe hao ni kiungo muhimu kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na wananchi.
“Kuweni karibu na Mahakama hapa Songwe na msome miongozo mbalimbali inayotolewa na kuielewa ili iwasaidie katika kuwalea Mahakimu wetu katika maadili yapasayo na pia kufahamu mipaka ya Mahakama pale mnapotekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa sheria”, alisema Jaji Mkuu.
Aidha aliwashauri Wenyeviti wa Kamati za Maadili za Mkoa na wilaya kuitisha vikao kwa mujibu wa sheria ili kujadili changamoto mbalimbali za Mahakama ikiwemo ya ukosefu wa majengo na kutoa mapendekezo ya maeneo yanayofaa kujengwa majengo mapya ya Mahakama.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza ziara yao katika mikoa ya Iringa, Njombe,Mbeya na Songwe mwishoni mwa wiki. Lengo la ziara hiyo ya siku tano kwenye mikoa hiyo ni kuitangaza Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na kutoa elimu kwa wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya na wadau wa Mahakama.