Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama,akizungumza leo Agosti 16,2021 na wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kikao kilichohusu kuwasaidia Wavuvi kukabiliana na changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao pamoja kuvipatia vyama vya ushirika vya uvuvi mikopo ili viweze kujiendesha.
Mkurugenzi wa Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Dkt Nazael Madalla,akiwasilisha mada wakati wa kikao hicho.
Katibu Mkuu Sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatama,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukutana na wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuwasaidia Wavuvi kukabiliana na changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao pamoja kuvipatia vyama vya ushirika vya uvuvi mikopo ili viweze kujiendesha.
……………………………………………………………………………………
Na Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) kuisaidia katika mambo matatu ikiwemo kuwaondoa wavuvi kutoka kwenye uvuvi wa maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboto ya kisasa badala ya mitumbwi na ngarawa.
Pia kuwasaidia kukabiliana na changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao pamoja kuvipatia vyama vya ushirika vya uvuvi mikopo ili viweze kujiendesha na kuwasaidia wavuvi.
Akizungumza leo Agosti 16,2021 na wajumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo,Frank Mugeta,Katibu Mkuu huyo amesema uvuvi wa samaki katika ukanda wa bahari unaweza kuongezeka iwapo wataweza kuwasaidia wavuvi katika mambo mbalimbali.
Pia, kuwaondoa wavuvi wadogo wadogo kutoka kwenye uvuvi wa maji ya ndani na kuwapeleka kuvua kwenye maji ya Kitaifa kwa kutumia maboto ya kisasa badala ya mitumbwi na ngarawa ambazo wengi wao bado wanazitumia.
“Sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza kutekeleza baadhi ya mikakati kuwawezesha wafugaji samaki wadogo kwenye maji ya asili kukabilina na changamoto za uwekezaji mdogo katika maeneo yao lakini hapo bado tuna changamoto,”amesema.
Amesema mafanikio katika utekelezaji wa mikakati yanategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa Taasisi za kifedha za ndani pamoja na nje.
Amesema Wizara imeanzisha dawati la sekta binafsi ili kuratibu upatikanaji wa mikopo kwa vyama vya ushirikia kwa kuyafanyia marekebisho maandiko yao ili yakidhi matakwa ya Kibenki.
“Kufikia Februari 2021,dawati lilimewezesha kupokelewa kwa maombi ya mikopo ya uvuvi katika Benki ya TADB yenye thamani ya shilingi bilioni 51.4 lakini kiasi kilichotolewa hadi sasa ni shilingi bilioni 1.2 kwa vyama vya ushirika vitatu katika Wilaya ya Ukerewe,Buchosa na Chato,”amesema.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TADB,Mugeta amesema mara baada ya kikao hicho wataenda kuangalia namna ya kuisaidia sekta hiyo ambayo inaajiri watanzania wengi.
Amesema wataisaidia sekta hiyo kutokana na kufanyika kwa tafiti nyingi ambazo zitawaongoza wao wasaidie sehemu zipi ili kuhakikisha Mtanzania anaweza kujikwamua kimaisha.
“Niahidi wataalamu wetu watakaa hili ni eneo la kusapoti kwa nguvu zetu zote nimeteuliwa nina siku 10 bado nina nguvu hivyo tutapata majawabu ya haraka ili tuone tunaanzia wapi.Tunataka kuhakikisha sekta ya uvuvi inaajiri watu wengi nafikiri ni eneo ambalo tutaliangalia kwa kina zaidi,”amesema.
Awali akitoa wasilisho kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Mkurugenzi wa Ukuzaji viumbe maji kutoka Wizara hiyo,Dkt Nazael Madalla amesema uvuvi ni miongoni mwa sekta zinazoajiri watu wengi wa kipato cha chini ambapo moja kwa moja takribani wavuvi na wakuzaji viumbe maji wapatao 225,435.
Amesema zaidi ya watanzania milioni 4.5 wameendelea kupata kipato cha kila siku kutokana na shughuli zinazohusiana na sekta ya uvuvi ikiwemo kuunda na kutengeneza boti,kuuza na kushona nyavu kutengeneza na kuuza barafu,biashara ya samaki na mazao yake.
Mkurugenzi huyo amesema sekta hiyo inachangia katika lishe na usalama wa chakula ambapo takribani asilimia 30 ya protein itokanayo na wanyama inachangiwa na samaki.
Amesema kwa upande wa kipato na fedha za kigeni katika mwaka 2021-2021 tani 483,756.4 zilivunwa na kuingiza kipato cha shilingi trilioni 2.42 kati ya mavuno hayo tani 41,319.00 na samaki hai wa mapambo 165,413 wenye thamani ya shilingi bilioni 18.91.
Mkurugenzi huyo amesema sekta hiyo ni muhimu kwani inachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.7
Amesema kwa sasa kiasi cha rasilimali za samaki kwenye maji ni zaidi ya tani nne ambapo amedai kiasi kinachoweza kuvunwa bila kuathiri mazingira ni tani 750,000.