Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaongoza wa Washiriki wa Mbio za CRDB International Marathon na kufanya mazoezi ya viungo, katika viwanja vya The Green, Jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaongoza wa Washiriki wa Mbio za CRDB International Marathon katika matembezi ya Kilomita 5, Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akivishwa medani ya ushiriki wa mbio za CRDB International Marathon na Mwenyekiti wa bodi ya CRDB, Dkt. Ally Lady, katika viwanja vya The Green, jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimkabidhi hundi, mshindi wa kwanza Kilimota 42 Wanawake, Shelmith Nyawira baada ya kumaliza mbio za CRDB International Marathon, katika viwanja vya The Green, jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi, mshindi wa kwanza Kilimota 65 Baiskeli Wanawake, Swabra Abdallah wakati wa mbio za CRDB International Marathon, katika viwanja vya The Green, jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Mohamed Janabi, hundi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya kusaidia upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo, wakati wa mbio za CRDB International Marathon, katika viwanja vya The Green, jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaisalage, hundi ya Shilingi milioni 104 kwa ajili kusaidia ujenzi wa kituo cha mawasiliano kwa wateja wakati mbio za CRDB International Marathon, katika viwanja vya The Green, jijini Dar es Salaam, Agosti 15, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza wizara zote zinazohusika na uratibu na uandaaji wa Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) wahakikishe wanakutana na kuweka mpango wa kurejesha michezo hiyo ili watumishi wa umma wapate fursa ya kushiriki na kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
Amesema michezo hiyo ya SHIMIWI ni muhimu kwa sababu ilikuwa inawakutanisha Watumishi wa Wizara za Serikali na Taasisi zake na ilisaidia sana kuboresha afya zao na kuongeza hamasa ya utendaji kazi hivyo kuongeza tija na ufanisi wa kazi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Agosti 15, 2021) wakati alipomuwakilisha Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za hisani za “CRDB Bank Marathon” zilizofanyika katika viwanja vya The Greens, Oysterbay Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema mashindano hayo ya SHIMIWI yaliwasaidia watumishi wa umma kupambana na magonjwa sugu yasiyoambukiza tofauti na sasa. “Nakumbuka mara ya mwisho michezo hii ilifanyika mwaka 2014.”
“…Naelekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuweka mikakati ya pamoja ya kufufua michezo na ushiriki wa michezo kwa watumishi, wanafunzi na wananchi kwa ujumla.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza TAMISEMI ihakikisheni inasimamia kwa ukaribu ushiriki wa michezo kwa watumishi na wananchi, pia michezo kama vile jogging, marathon, mchakamchaka nayo inatakiwa ipewe kipaumbele hususan kwa wanafunzi.
“Natambua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ni wenyeviti wa Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya katika maeneo yao. Kwa hiyo, hakikisheni mnalisimamia jambo hilo.”
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali kwa upande wake imeruhusu shughuli za michezo ziendelea kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha afya za binadamu pamoja na kujikinga na ugonjwa wa UVIKO19. “Mazoezi kama ilivyo lishe ni muhimu sana kwenye kulinda mwili dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo UVIKO19.”
Waziri Mkuu amesema kwa upande huo wa mazoezi, Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri watu wafanye mazoezi ya walau dakika 150 kwa wiki (yaani dk 30 kila siku kwa siku 5 za juma). “Haya ni mazoezi ya kiwango cha chini kama vile kutembea, kuendesha baiskeli.”
“Kwa msingi huo, binafsi ninafarijika sana kuona mwitikio huu mkubwa kutoka kwa Watanzania pamoja na wageni kwenye tukio hili adhimu. Kwa lugha nyingine, ushiriki wenu kwenye mbio hizi za CRDB Bank Marathon ni kielelezo tosha kuhusu utayari na utu mlionao katika kuchangia watoto wetu kupata huduma za upasuaji wa moyo.”
Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango huo katika kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi wa watoto hawa. “Nyote mtakubaliana nami kuwa kuuguza si jambo la lelemama hasa unapouguza mtoto. Jambo la kuuguza mtoto husababisha wasiwasi na maumivu kwa wazazi na walezi hasa tunapokuwa tukishuhudia watoto wetu wakiugulia maumivu ya ugonjwa.”
“Nimefahamishwa kuwa ushiriki wenu kwenye mbio hizi, utawezesha upatikanaji wa fedha za kuanzisha Kituo cha Taarifa za Saratani (Cancer Information Centre) katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road. Kituo hiki kitakuwa kiungo muhimu kati ya wagonjwa wa saratani, wanaohudumia wagonjwa wa saratani na wale wenye wasiwasi juu ya saratani.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema hii ni mara ya pili kwa benki hiyo kuandaa mbio hizo, Agosti mwaka jana ambapo zaidi ya watu 4,000 walichangia watoto 100 kupata tiba ya upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa gharama ya shilingi milioni 200.
Alisema lengo la mbio za mwaka huu ni kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kuanzisha Kituo cha Taarifa za Saratani (Cancer Information Centre) katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na kuimarisha afya zao kwa kufanya mazoezi huku wakijumuika na familia, rafiki na jamii.