Sehemu ya mashine za kutengenezea matairi
Waziri wa Viwanda na Biashara Kitila Mkumbo akiwa na viongozi wengine wakikagua kiwanda hicho cha kutengeneza matairi kikagua mashine za kutengenezea matairi
Waziri wa Viwanda na biashara akibadilishana mawazo mara baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho.
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof Kitila Mkumbo (katikati)akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mkakati wa Serikali katika kiwanda cha General Tyre.
………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu,Arusha
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali ipo katika mchakato wa kukiuhisha kiwanda cha General Tyre cha Arusha kwa lengo la kuona uzalishaji wa matairi kiwandani hapo zinaanza tena.
Profesa Mkumbo aliyasema hayo wakati alipofanya ziara katika kiwanda hicho kilichoacha kufanya uzalisha kwa muda wa zaidi ya miaka 10 kutokana na teknolojia ya uzalishaji kupitwa na wakati pamoja na matairi yaliyokuwa yamezalishwa kukosa soko.
Ambapo amesema kuwa lengo la kufanya eneo hilo kuwa mtaa wa viwanda ni kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuleta ajira kwa watanzania hasa watu wa Arusha.Amesema kuwa wamechagua maeneo machache yatakayoweza kuanzisha mitaa ya viwanda ambayo yataweza kuleta tija nchi nzima .
Hivyo kwa kuanzia wamechagua Mikoa ya
Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha ambapo kwa Arusha wamechagua eneo la General tyre ambapo ndani yake kutakuwa na viwanda vikubwa na vidogo.
Amefafanua kuwa watafanya upembuzi yakinifu kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo(NDC) ili waweze kupata ushauri wa kitaalamu na ni aina gani ya viwanda vinaweza kukaa katika eneo hilo na kwa kuzingatia uzuri wa mji wa Arusha.
“Niwaambie wananchi wa Arusha kuwa ni kweli kiwanda hiki kiliacha kufanya uzalishaji tangu mwaka 2007 na kupoteza ajira zaidi ya 400 lakini katika muda mfupi ujao kupitia uongozi wa Muheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu tutaenda kutumia eneo hili vizuri kupata mtaa wa viwanda vya kueleweka ndani ya eneo hili na naamini litachochea maendeleo ya nchi,” amesema. Profesa Kitila.
Ameongeza kuwa mitambo iliyopo katika kiwanda hicho haviwezi tena kufanya kazi ya kuzalisha matairi kutokana na kupitwa na wakati hali ambayo haitaweza kuzalisha matairi yatakayoendana na uhitaji wa soko la hivi sasa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la NDC Rhobi Sattima amesema uzalishaji wa tairi unahitaji eneo kubwa zaidi ya ekari 200 lakini eneo hilo lina ukubwa wa ekari 50 ambapo wamefanya utafiti katika viwanda vingine vya nje ambavyo pia vinatumia eneo kubwa hivyo kufanya eneo kukosa mwekezaji kwaaji ya uzalishaji huo.
Aidha Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema kuna changamoto kubwa ya ajira na wanaamini kufufuka kwa kiwanda hicho kutatoa mwanga wa serikali ya awamu ya sita ili wananchi wa Arusha waweze kupata ajira na serikali iweze kupata kodi zitakazotokana na uzalishaji utakaokuwepo.
“Sisi wananchi wa Arusha tuna shauku kubwa na kuendelezwa kwa kiwanda hiki, ambapo matarajio yangu kuendelezwa kwa eneo hili halita chukua muda ili wananchi wangu waweze kupata ajira hapa na serikali ipate mapato,” amesema Gambo