Waziri wa Madini Dotto Biteko kushoto na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge kulia,wakimsikiliza jana mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi katikati wakati wa ziara ya Waziri wa madini alipotembelea mgodi huo ili kujionea kazi zinafanywa na mwekezaji huyo.
Mmiliki wa mgodi wa dhahabu Lukalasi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Jonson Nchimbi kulia,akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa dhahabu kwa Waziri wa Madini Dotto Biteko katikati, aliyetembelea mgodi huo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge.
Picha na Muhidin Amri,
*****************************************
Na Muhidin Amri,
Mbinga
WAZIRI wa madini Dotto Biteko, ametembelea mgodi wa dhahabu wa Lukalasi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma unaomilikiwa na mzawa Jonson Nchimbi na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na mwekezaji huyo.
Waziri Biteko amesema, wizara ya madini itaendelea kumuunga mkono mwekezaji huyo mzawa katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini.
Kwa mujibu wa Waziri Biteko, katika kipindi kifupi mwekezaji huyo amechimba dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 3 na amelipa zaidi ya Sh milioni 200 kama kodi kwa Serikali.
Amewaomba wananchi wanaofanya kazi katika mgodi huo kufanya kazi kwa uaminifu na kujiepusha na vitendo vya wizi vinavyoweza kumvunja moyo mwekezaji huyo mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma.
Amesema, haya madini ni nyenzo pekee ambaye Watanzania tumepewa na Mungu ili tuondoa umaskini wetu,kwa hiyo ni lazima tuchimbe kwa haki,kulipa kodi na kufuata sheria na taratibu za nchi badala ya kutugombanisha.
Waziri Biteko amesema,kwa kutambua uwekezaji huo, Serikali itaendelea kumsaidia kwa kumpatia wataalam ili aweze kuchimba dhahabu kisasa na kumkutanisha na taasisi mbalimbali za fedha ili kupata mikopo.
Amesema, lengo ni kumwezesha kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini kwa sababu bado ana vifaa vya kizamani.
Amesema, serikali inatambua leseni zote na baadhi bado hazijafanyiwa kazi na nyingine zimeisha muda wake, hivyo wizara ya madini itazifuta ili kupewa watu wengine watakaokuwa tayari kuchimba na kuachana na watu wenye tabia ya kushikilia maeneo bila ya kuyafanyia kazi.
Amesema,uchimbaji wa madini ni safari ndefu na serikali inawahitaji sana wachimbaji wakubwa na wadogo na kamwe wizara haitaruhusu kuwepo kwa wachimbaji wakubwa pekee yake kwani inahitaji watu wengi kufanya utafiti ili kufahamu kiasi cha madini kilichopo katika nchi yetu.
Ameiagiza,ofisi ya Mkuu wa Ruvuma na mkuu wa wilaya Mbinga kuhakikisha inapitia upya maeneo na leseni zote ambazo hazijaendelezwa ili maeneo hayo yaweze kupewa vikundi vidogo kwa ajili ya uchimbaji.
Mmiliki wa mgodi huo Jonson Nchimbi amesema,tangu mgodi ulipoanzishwa wameweza kuzalisha dhahabu yenye thamani ya Sh.bilioni 3,038,167,518.24 na kulipa mrabaha wa Sh.182,290,051.09,ada ya ukaguzi Sh. Milioni 30,381,675.18 pamoja na ushuru wa Halmashauri jumla ya Sh.9,114502.55.
Aidha amesema,mgodi unashiriki shughuli mbalimbali za kijamii na za maendeleo katika kijiji cha Lukalasi na umetoa ajira kwa wananchi wasiopungua 300 wanaofanya kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa dhahabu juu ya ardhi.
Hata hivyo amesema, kwa kuwa eneo hilo limeanza kujulikana kuwa na uzalishaji mzuri wa dhahabu kumeanza kutokea migogoro michache ya kuingiliana katika leseni za uchimbaji na kuishukuru wizara ya madini kumaliza moja kati ya migogoro hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge amesema,serikali inatambua uwezo wa mgodi huo katika kuongeza ajira na mapato ya serikali na mapato binafsi.
Balozi Ibuge,amewataka wananchi wanaishi kuzunguka mgodi huo kutambua juhudi za uwekezaji na kazi inayofanyika katika mgodi huo ambao tangu ulipoanzishwa umeshaleta manufaa makubwa.
Hata hivyo,ametaka kufanyiwa kazi tatizo la kushuka kwa uzalishaji wa dhahabu katika mkoa huo ambapo kwa Mwezi Julai dhahabu iliyopatikana ni kilo 2,wakati mwezi Juni ilikuwa kilo 4, na Mwezi Mei kilo 5.
Amesema, serikali ya mkoa itaendelea kuunda vikundi vingi na kuwataka viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Ruvuma kuhamasisha wanachama wake kwa kuwa lengo la Serikali ya mkoa ni kutoa ajira na kuongeza mapato yatokanayo na madini.