Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa wakandarasi na wahandisi washauri wanaotekeleza ujenzi wa barabara ya Njombe – Moronga – Makete (km 107.4) kwa kiwango cha lami mara baada ya kukagua mradi huo, mkoani Njombe.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalua, akitoa taarifa ya mradi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa barabara Njombe – Moronga – Makete (km 107.4) kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akikagua sehemu ya barabara ya Moronga – Makete (km 53.5) inayojengwa kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake umefikia asilimia 69, mkoani Njombe.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete (km 96.4); ambayo Serikali imekwisha tangaza zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi sehemu ya barabara ya Kitulo hadi Kidope (km 25). Ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utaunganisha mkoa wa Mbeya na Njombe na kufungua fursa za kiuchumi na kiutalii.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Njombe – Moronga (km 53.9) inayojengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi China Henan International Cooperation Group ambao ujenzi wake umefikia asilimia 89 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Moronga – Makete (km 53.5) inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi China Railway Seventh Group ambao ujenzi wake umefikia asilimia 69.
PICHA NA WUU
********************************
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema kuwa imekwisha tangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete; sehemu ya Kitulo hadi Kidope (km 25) inayounganisha mkoa wa Mbeya na Njombe kwa ajili ya kufungua fursa za kiuchumi na kiutalii katika mikoa hiyo.
Aidha, Wizara imeahidi kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia sehemu iliyobaki ya barabara hiyo yenye jumla ya urefu wa kilometa 96.4.
Hayo yamesemwa mkoani Njombe na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Njombe – Moronga – Makete (km 107.4) zinazojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ameridhishwa na hatua ya miradi huo unaoendelea kutekelezwa.
“Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao kama vile viazi na miti ya mbao lakini pia inapita katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo yenye vivutio vingi hivyo Serikali imeamua kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami”, amefafanua Naibu Waziri Kasekenya.
Kuhusu suala la malipo ya wakandarasi nchini, Naibu Waziri Kasekenya amesema kuwa mpaka sasa hakuna mkandarasi anayeidai Serikali kwa upande wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja kwani Serikali imekwisha lipa madai yao na maeneo mengi kazi zinaendelea.
“Niwatake wakandarasi wote nchini wasituangushe kwa kuwa Serikali imejipanga na fedha zinatolewa kwa wakati hivyo ni jukumu lao kukamilisha miradi yote kwa wakati na kimkataba”, amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya ametoa wito kwa viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya na Mkoa kusimamia miundombinu ya barabara na madaraja inayojengwa kwa fedha nyingi kwa kuhakikisha haihujumiwi na kutunzwa kwa hali na mali.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe, Mhandisi Ruth Shalua, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa ujenzi wa barabara ya Njombe – Moronga (km 53.9) umefikia asilimia 89 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu, wakati sehemu ya barabara ya Moronga – Makete (km 53.5) ujenzi wake umefikia asilimia 69.
Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Njombe – Moronga (km 53.9) kwa kiwango cha lami unatekelezwa na Mkandarasi China Henan Internation Corporation kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 107 na sehemu ya ujenzi wa barabara ya Moronga – Makete (km 53.5) kwa kiwango cha lami unatekelezwa na mkandarasi China Railway Seventh Group kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 110 ikiwa zote ni fedha za Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi