*********************************
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kusimamisha uchapishaji wa gazeti la Uhuru kwa siku saba kuanzia leo Jumatano kwa kuandika habari ya kupotosha juu ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Kupitia gazeti hilo nakala ya leo lilionekana kumlisha maneno Mwenyekiti huyo wa chama Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Chama hicho Lumumba Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Daniel Chongolo amesema kupitia kwa makosa yaliyojitokeza wanamuomba radhi Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.
“Tunamuomba radhi Rais kwa kumlisha maneno, ukifuatilia mahojiano yoyote BBC hakuna sehemu amezungumza na muungwana ni vitendo. Tayari bodi imewasimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji, Ernest Sungura, Mhariri mtendaji na Rashid Zahoro ambaye alikuwa msimamizi gazeti”. Amesema Mhe.Chongolo.