************************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Kaya masikini katika vijiji 22 wilayani Ludewa mkoani Njombe zinatarajia kunufaika na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ambacho kimeboresha uendeshaji wa mfumo wake ambapo kwa sasa malipo yatafanyika kwa njia ya kielekroniki na usajili wa wanufaika hao utatumia kitambulisho cha Taifa.
Mfuko huo katika awamu iliyopita ulizifikia kaya masikini kwa asilimia 70% nchi nzima na kubakiza asilimia 30% ambapo kwa Ludewa vilifikiwa vijiji 55 na kubakia vijiji 22 ambapo kwa sasa watapata malipo kwa kutumia simu zao, mawakala pamoja na bank badala ya utaratibu ule wa awali wa kulipa mkononi hivyo wanufaika wote wanatakiwa kuwa na namba au kitambulisho cha Taifa.
Akizungumza katika uzinduzi wa kikao kazi cha kujenga uelewa muwezeshaji ngazi ya Taifa Ally Mwamia ambaye alimuwakilisha mkurugenzi wa mfuko huo amesema wameamua kuboresha mfuko huo kutokana na kutokea kesi nyingi za walengwa kutopata fedha ipasavyo sambamba na kupata taarifa sahihi za wanufaika hao.
Ameongeza kuwa kulikuwa na tabia ya kuchukuliana fedha na kuwafikishia walengwa fedha pungufu au kutowafikishia kabisa pia hata kwa baadhi ya wasimamizi kutotoa taarifa pindi mnufaika anapofariki na kupelekea fedha hizo kuishia katika mikono yao na watu wengine hivyo kwa sasa wanufaika hao wanapaswa kuwa na kitambulisho hicho cha Taifa na pasipo kitambulisho au namba hawataweza kupata usajili.
“Kuna baadhi ya kaya unakuta mnufaika yuko peke yake bila mrithi yeyote hivyo anapofariki inamaana hakuna wakuchukua tena fedha lakini kamati zetu hizi zinaendelea kupokea fedha na kwakuwa wanasaini kwa dole gumba ndipo unagundua midole ya aina tofauti tofauti katika jina moja”, alisema Mwamia.
Kwa upande wa mkuu wa wilaya ambaye aliwakilishwa na katibu tarafa wa mwambao Linus Malamba amewataka wawezesha kutenda haki katika kuandikisha kaya hizo ili fedha hizo ziwafikie kaya masikini na si kwa watu wenye uwezo.
Amesema kufanya kazi kwa weledi ndiyo nguzo pekee itakayowawezesha kutenda haki hiyo hivyo walengwa ndio watakaonufaika na si vinginevyo.
Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Wise Mgina ambaye pia ni diwani wa kata ya Mundindi amewapongezaTASAF kwa kuwashirikisha madiwani katika kuwajengea uelewa huo kwani awali hawakushirikishwa na kupelekea kushindwa kuwasaidia wananchi wa kaya hizo wanapokuwa na hoja mbalimbali juu ya mfuko huo.
Ameongeza kwa kuwaomba watambuzi wanaoenda kuzitambua kaya hizo kuwapa elimu pia wanufaika juu ya matumizi mazuri ya fedha wanazopata badala ya kuwapa na kuwaacha kitu ambacho kinapelekea baadhi yao kufanya matumizi yasiyo sahihi na kuwafanya waendelee kuwa masikini.
Naye Tekla Hongoli ni afisa maendeleo ya jamii kata ya Ludewa ambaye ni mmoja wa watambuzi wa kaya masikini amesema mfumo huu wa sasa ni mzuri lakini kwa walengwa itakuwa ni changamoto katika kutumia mfumo huo.
Amesema kumekuwa na changamoto katika upataji vitamvulisho vya taifa hivyo anaona kuna baadhi ya kaya zinaweza kukosa msaada huo sambamba na wengi wao kutokuwa na simu, kushindwa kutumia mifumo ya kibenki hivyo kwa sasa watakuwa na wakati mgumu katika kuandikisha kaya hizo.