…………………………………………………………………….
Na.Faustine Gimu Galafoni,Mwanza.
Katika kuhakikisha vipaji mbalimbali vinaibuliwa na kuendelezwa,serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo inatarajia kujenga kituo mahiri cha kwanza cha kukuza na kulea vipaji hapa nchini kitakachojengwa katika chuo pekee cha Maendeleo ya Michezo kilichopo Malya Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza.
Akizungumza na Mtandao huu ,Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Richard Mganga amesema kituo hicho mahiri kitagharimu Tsh.Bilioni 1.3 na kitaleta fursa ya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana hapa nchini.
“kwa mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetenga fedha Tsh.bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kulea na kukuza vipaji Malya,tumeona vijana wamekuwa wakimaliza Mashindano ya UMISETA NA UMITASHUMITA shuleni lakini wanakosa waelekee wapi hivyo kupitia kituo hiki kitasaidia vijana kuendeleza vipaji vyao”amesema Mganga
Aidha,Mganga katika kituo hicho kutakuwa na miundombinu mbalimbali itakayowajengea uwezo vijana katika kuibua vipaji vyao.
“Tutakuwa na miundombinu ya viwanja,Swimming Pool kiwango cha kimataifa,Mpira wa wavu watalelewa hapa,mpira wa pete,kikapu watalelewa hapa na itakuwa sehemu ya kuzalisha ajira mbalimbali”amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya akiwemo Ramadhan Salum pamoja na Anita Mlay amesema kituo hicho cha kulelea na kukuza vipaji Tanzania ambacho kitakuwa cha kwanza hapa nchini kitaleta chachu kubwa katika kuinua vipaji vya vijana Tanzania.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Chuo amesema Serikali imeshatoa Jumla ya Tsh.Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya kisasa katika chuo hicho na kukiwa na mahitaji ya Tsh.Bilioni 2.9 mpaka kukamilika kwake ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 192.
“Mpaka sasa tumeshapokea Tsh.Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 192 na kila chumba kutakuwa na wanafunzi wasiozidi wane kiuhalisia ni hosteli kubwa”amesema.
Naye Mkurugenzi wa Michezo kutoka Wizara ya Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Yusuf Singo alisema mwezi huu huu Agosti,mwaka 2021 Serikali inatarajia kuzindua mpango mkakati wa taifa wa kutoa mwelekeo wa michezo ambao unaambatana na uboreshaji wa miundombinu .