Dk Benedicta Masanja Mkuu wa Mradi wa Uhuru wa USAID, akikabidhi moja ya kifaa cha maabara cha Gene Xpert. Mh. Cosmas Nshenye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Omary Mgumba iliyotolewa na Serikali ya Marekani kupitia USAID.
…………………………………………………………………………
Songwe,
Serikali ya Marekani, kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limekabidhi vifaa vya maabara kwa ajili ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu vyenye thamani ya TZS 424,361,043 (Dola za Marekani 182,993) kwa vituo 19 vya afya katika mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa, na Songwe. Vifaa hivyo vitaimarisha uwezo wa uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB), kuongeza utambuzi wa wagonjwa wa kifua kikuu na hivyo kuchangia udhibiti wa kifua kikuu nchini Tanzania. Mikoa hii minne inasaidiwa na Mradi wa Uhuru unaofanya shughuli zake za huduma za Kifua Kikuu na Uzazi wa mpango katika vituo vya afya kwa ufadhili wa USAID kupitia Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali ya hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Health Promotion Support (THPS), Dk Redempta Mbatia, amekabidhi mashine nane za GeneXpert na hadubini 11 za iLED kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba, ambaye alipokea vifaa hivyo kwa niaba ya mikoa yote minne. Hafla hiyo ilifanyika katika Zahanati ya Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW); Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma, Mtaalamu wa Teknolojia ya Maabara wa Mkoa; na Waganga wa Wilaya za Mbozi na Tunduma. Vifaa hivi vilivyotolewa vitatumika katika vituo vya afya vyenye wagonjwa wengi kulingana na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa afya wa mikoa. Tanzania ni moja kati ya nchi 30 zenye wagonjwa wengi wa kifua kikuu duniani. Mradi wa Uhuru TB na FP LON wa USAID unakusudia kuboresha upatikanaji wa huduma bora za Kifua Kikuu na uzazi wa mpango kwa lengo la kuongeza afya za wananchi katika mikoa wa Katavi, Kigoma, Rukwa, na Songwe. Kabla ya ufadhili huu, mikoa hii minne ilikuwa na mashine 16 tu za GeneXpert na hadubini 13 za iLED zilizokuwa zikihudumia idadi ya watu karibu milioni 6. Hali hii ilisababisha huduma duni za utambuzi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa jamii. Vifaa vya utambuzi vya GeneXpert hupunguza muda wa uchunguzi wa kifua kikuu kutoka wiki mbili hadi tatu hadi dakika 90 – 120. Aidha hadubini za iLED zitatumika kuongeza utambuzi wa wagonjwa wa TB katika vituo visivyo na mashine za GeneXpert.
Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, V. Kate Somvongsiri alisema “Mashine nane za GeneXpert na hadubini 11 za iLED ni sehemu ya mchango wa USAID katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa maabara za kifua kikuu nchini Tanzania. Vifaa hivi vinatarajiwa kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wa kifua kikuu na hususan kwa makundi ya kijamii yasiyofikika kirahisi kwa lengo la kupunguza tofauti ya usawa kwenye huduma za TB. Ili kutimiza azma ya nchi kumaliza kifua kikuu ifikapo mwaka 2030, wagonjwa wanapaswa kutambuliwa kwa wakati na matibabu kuanzishwa mapema.”
THPS ni shirika lisilo la kiserikali nchini Tanzania, linatekeleza mradi huu kwa kushirikiana na Baylor Tanzania, MKUTA, na Taasisi ya Afya ya Ifakara. THPS pia inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya afya Maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Wizara ya Mambo ya Ndani; na Wizara ya Afya Zanzibar hii yote ni katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa Watanzania. Kazi yao ni pamoja na kuimarisha mifumo ya afya na huduma za jamii kwa ujumla wake na kwa ubora unaotakiwa. Shughuli hizi zinalenga magonjwa ya VVU / UKIMWI; kifua kikuu; masuala ya kuzuia ukatili wa kijinsia; huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, na huduma za afya kwa vijana walio katika rika balehe; na mifumo ya taarifa ya usimamizi wa maabara na afya.