*****************************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Imeelezwa kuwa kutokana na uhaba wa watumishi katikati idara ya ardhi wilayani Ludewa mkoani Njombe imepelekea kushindwa kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati ambapo zaidi ya vijiji 14 kati ya 77 vilivyopo wilayani humo migogoro yake haijatatuliwa.
Hayo ameyasema diwani wa kata Milo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya huduma za uchumi, ujenzi na mazingira wakati akijubu swali lililoulizwa na diwani wa kata ya Iwela Joackim Lukuwi juu ya lini serikali itamaliza migogoro hiyo.
Amesema idara hiyo ya ardhi ina upungufu wa watumushi ambapo imekuwa ni vigumu kujigawa katika kutimiza majukumu hayo huku akimuomba mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutoa majibu ya nyongeza.
Akitoa majibu zaidi afisa utumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo Gladness Mwano ambaye ali kaimu nafasi ya mkurugenzi Sunday Deogratias amevitaja vijiji hivyo vyenye migogoro kuwa ni Iwela na Mbongo, Iwela na Nkomang’ombe, Nsungu na Kingole, Ibumi na Amani, Mavanga na Njelela, Mbugani na Mundindi, Luana na Milo pamoja na Ludende.
Amesema kuwa pamoja na uhaba huo wa watumishi lakini idara hiyo imejipanga kumaliza migogoro hiyo ambapo mpaka kufikia mwezi Agosti mwaka huu wanatarajia kumaliza migogoro hiyo.
” Pamoja na kwamba tunaupungufu wa watumishi katika idara ya ardhi lakini haituzuii kufanya kazi na kutimiza wajibu wetu hivyo kwa uchache huohuo wa watumishi tutahakikisha migogoro hiyo inamalizika na kila kijiji kitajua mipaka yake”, alisema Bi. Mwano.
Aidha kwa upande wa afisa mipango miji wa wilaya hiyo Issac Makinda amesema watendaji ni wachache na shuguli zimekuwa nyingi hivyo ili kufanikisha suala hili wanalazimika kusimamisha shuguli nyingine ambazo ni endelevu na kushughulika na suala moja.
Amesema hata hivyo kuna baadhi ya vijiji tayari utatuzi wake ulishaanza na kufikia hatua ya utambuzi wa mipaka huku baadhi ya maeneo yakiwa ni mapya ambayo yameanzishwa shuguli za mashamba na kuhitaji upimwaji.
“Migogoro hii ya mipaka inatulazimu kusimamisha shuguli nyingine ambazo ni endelevu kama upimaji wa kutoa hati miliki kwa wananchi, kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na nyinginezo hivyo ili kutatua kero hizo ni lazima shuguli nyingine zisimame”, Alisema Makinda.
Wise Mgina ni diwani wa kata ya Mundindi lakini pia ni mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amemuagiza mkurugenzi kumaliza migogoro hiyo kwa kipindi hicho cha mwezi Agosti mwaka huu sambamba na kuleta taarifa ya utatuzi huo katikati kikao kijacho cha baraza.
Ameongeza kuwa migogoro hiyo ni ya muda mrefu hivyo inapelekea wananchi kupoteza muda wao ambao wangeweza kufanya shuguli nyingine lakini wanalazimika kuutumia kwenye migogoro hiyo.