Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii) Dkt. Christopher Timbuka akizungumza na askari wa Mamlaka hiyo (hawapo pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya askari wanyamapori duniani.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii) Dkt. Christopher Timbuka (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa askari wanyamapori Bw. Pius Rwiza kama motisha ya kutambua mchango wake katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na misitu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Huduma za Ulinzi NCAA Bw. Elibariki Bajuta akizungumzia umuhimu wa maadhimisho ya siku ya wanyamapori duniani wakati halfa fupi ya kuwapongeza askari wa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu mkoani Arusha.
Askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika mazoezi ya vitendo wakati wa maadhimisho ya siku ya askari Wanyamapori iliyofanyika ofisi za NCAA Karatu Mkoani Arusha.
Sehemu ya menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika picha ya pamoja na askari ya mamlaka hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya askari wanyamapori duniani iliyofanyika katika ofisi za NCAA Wilayani Karatu Mkoani Arusha.
……………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu NCAA.
Tarehe 31 Julai ya kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya askari wanyamapori duniani (World Rangers day) ikiwa ni kumbukumbu ya kuwaenzi askari waliopoteza maisha wakiwa kwenye utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usimamizi wa wanyamapori.
Katika kuadhimisha siku hiyo Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Dkt. Christopher Timbuka wamekutana na askari wanyamapori wa Mamlaka hiyo kwa lengo la kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazowakabili pamoja na kutambua kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.
“Maadhimisho ya siku hii ni sehemu ya kutambua mchango wa askari wanaolinda rasilimali za wanyamapori na misitu, wapo waliopata madhara katika kazi hii hivyo ni muhimu kuwatambua na kuwapa moyo, pamoja na changamoto wanazopitia tunawasisitiza kuendelea kuchapa kazi kwa kuweka uzalendo, bidii, uaminifu, uadilifu na ujasiri kama nguzo muhimu katika uhifadhi wa rasilimali za misitu na wanyamapori” alisisitiza Dkt. Timbuka.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Idara ya huduma za Ulinzi Elibariki Bajuta amebainisha kuwa NCAA imefanya maadhimisho ya siku hiyo kwa askari kufanya maonyesho mbalimbali na baadae kukutana na kukutana na uongozi wa shirika kwa ajili ya kuwapa moyo na kuwaahidi kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kutoa mafunzo na vitendea kazi vya kisasa vitakavyosaidia kufanya doria za miguu hasa katika mazingira magumu ya milima na misitu minene.
“Pamoja na kutambua mchango wao katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, NCAA itaendelea kutoa motisha ya mafunzo, stahiki mbalimbali na vitendea vya kisasa kuimarisha doria hasa maeneo yenye changamoto za milima, mabonde na misitu minene ili kuwatia moyo wa kuendelea kupigania rasilimali za wanyamapori na misitu.” amefafanua Bajuta.
Katika maadhimisho ya siku ya askari wanyamapori duniani jumla ya askari 9 wamepewa vyeti maalum kama sehemu ya kutambua mchango wao katika jitihada za ulinzi wa Wanyamapori katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.