**************************
Mahakama ya Hakimu mkazi Pwani (Kibaha) imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Ridhiki Omary Marimbwa kwa kosa la kusafirisha kilo 21.86 za dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hiyo ilitolewa tarehe 29 mwezi Julai 2021 na hakimu Mhe. Joyce Mushi baada ya mtuhumiwa kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha Dawa za kulevya aina ya bangi
Akisoma hukumu hiyo mheshimiwa Joyce Mushi amesema kwamba, upande wa Jamhuri umethibitisha kosa hilo pasi na kuacha shaka hivyo imemtia mshtakiwa hatiani. Kwa kuwa, makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya yamekithiri mkoani Pwani, hana budi kumpa mshtakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakati akijitetea mshtakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ana familia yenye watoto wadogo wanaomtegemea.
Pamoja na hukumu hiyo Mhe. Mushi aliamuru kutaifishwa kwa pikipiki iliyotumika kutekeleza uhalifu huo pamoja na kuteketezwa kwa bangi iliyokamatwa.
Mshtakiwa alikamatwa tarehe 18 mwezi Agosti mwaka 2020 kwenye hifadhi ya wanyamapori ya Selous mkoani Pwani akisafirisha dawa hizo.
Mshtakiwa ametiwa hatiani kwa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Imetolewa na,
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za Kulevya