Jengo la zahanati ya kijiji cha Kankwale Manispaa ya Sumbawanga ambalo limekamika kujengwa sasa baada ya kipindi cha miaka 17 tangu wananchi walipoanza mradi huo ambapo Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti ameagiza ifikapo mwezi Octoba mwaka huduma zianze kutolewa kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Bw. Jacob Mtalitinya akitoa maelezo ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Fyengeleza iliyokamilika baada ya miaka 8 tangu wananchi waanze kuijenga wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Joseph Mkirikiti ( hayupo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiongea na viongozi wa Wilaya ya Sumbawanga kuhusu aguzo la serikali kuona zahanati ya kijiji cha Fyengelezya ikamilike na kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Octoba jana huu
……………………………………………………………………
Zahanati mbili za vijiji vya Fyengeleza na Kankwale zilizoanzishwa ujenzi wake na wananchi na kukwama kwa zaidi ya miaka 17 sasa zimekamilika na zitaanza kutoa huduma kwa wananchi mwezi Octoba mwaka huu baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kuzikamilisha.
Akiwa katika ziara ya kukagua miradi katika Manispaa ya Sumbawanga, jana (29.07.2021) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti ameipongeza halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kazi nzuri ya kukamilisha miradi hiyo ya zahanati zilizokwama kwa kipindi kirefu.
Taarifa zilizosomwa katika miradi hiyo ya zahanati kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa zilieza kuwa Zahanati ya kijiji cha Kankwale ilianza kujengwa miaka kumi na Saba (17) iliyopita pale wananchi walipoanzisha ujenzi huo mwaka 2004 huku ile ya kijiji cha Fyengelezya ikichukua miaka minane (8) kukamilika kutokana na sababu nyingi ikiwemo usimamizi usioridhisha wa miradi na ukosefu wa fedha.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa zahanati ya Kankwale imegharimu kiasi cha shilingi 81,068,000/- kukamilishwa kati ya hizo nguvu za wananchi zinazotokana na michango ya fedha tasilimu na nguvu zao kiasi cha shilingi milioni 24 na Manispaa kupitia mapato yake ya ndani imetumia shilingi milioni 10 na kiasi cha shilingi milioni 50 kimetoka serikali kuu.
Imeelezwa kuwa Zahanati ya Fyengerezya hadi kukamilika imegharimu kiasi cha shilingi milioni 75 kati ya hizo Manispaa imechangia kiasi cha shilingi milioni 25 kutoka mapato yake ya ndani na shilingi Milioni 50 zimetolewa na serikali kuu.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti ameeleza kufurahishwa na ukamilishwaji wa Zahanati hizo zinazotoa jibu la ukosefu wa huduma kwa wananchi waliosubiri kwa muda mrefu na kuhoji miaka 17 nini kilikwamisha.
“Ninawapongeza viongozi wa Manispaa hii kwa jitihada na ubunifu wa kukamilisha majengo yaliyoanzishwa na wananchi kwa muda mrefu mfano zahanati ya Kankwale ilianza kujengwa mwaka 2004 huku ile ya Fyengeleza mwaka 2014 leo tunaona uongozi wa Manispaa wa sasa ukikamilisha kazi hii na kuwa mwezo Octoba huduma zitatolewa, ninachojiuliza ni swali hili, kwa nini miaka 17 hizi zahanati zilikwama? Ni ukosefu wa fedha kweli au ni usimamizi?”. alisema Mkirikiti.
Mkirikiti aliongeza kuwa jitihada za Manispaa hiyo kukamilisha ujenzi wa majengo ambayo yalijengwa na wananchi lakini hayakukamilika unatoa suluhisho la upungufu wa miundombinu ikiwemo shule mpya ya msingi Ntendo “B”, maabara za sayansi shule za sekondari Kalangasa na Ntendo.
“Wito wangu bado tunao mzigo ni mkubwa ndani ya manispaa yetu na mkoa wetu wa Rukwa ,hivyo tunapaswa kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuweza kunufaisha wananchi huku tukizingatia ubora na matumizi sahihi ya fedha za umma”. alisisitiza Mkirikiti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema mafanikio yaliyowezesha kukamilishwa kwa miundombinu hiyo ni ushirikiano waliopata toka kwa wananchi na watumishi wa halmshauri hiyo .
“Siri ya kukamilisha miradi hii imetokana na ushirikiano wetu ndani ya Manispaa wakiwemo Madiwani wetu na pia usimamizi wa miradi shirikishi pamoja na uwepo wa fedha toka Serikalini” alisema Mtalitinya.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Fyengeleza Frolence Masanja aliishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliokuwa umekwama miaka mingi.
Masanja alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia wananchi hususan akina mama wajawazito na watoto kupata huduma karibu zaidi na makazi yao tofauti na ilivyo sasa ikihusisha kusafiri kwenda mjini Sumbawanga.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye amehamishiwa Rukwa kutoka Mkoa wa Manyara hivi karibuni alibainisha lengo la Mkoa wake kuwa ni kuhakikisha majengo ya shule na zahanati yaliyokwama ujenzi wake yanakamilika kabla ya mwezi wa Octoba mwaka huu ili kuweza kuruhusu utoaji huduma za elimu na afya.
Mwisho
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
SUMBAWANGA
30.07.2021