Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi baada ya kutia saini kanuni za uendelezaji wa nishati mbadala.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro akikata utepe ili kuzindua kanuni za uendelezaji wa nishati mbadala. Wengine ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki kulia Dk.Ezekiel Mwakalukwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Do Santos Silayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro akitia saini kanuni za uendelezaji wa nishati mbadala.
……………………………………………
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro amewataka Watanzania kujipanga kutumia nishati ya mkaa mbadala ili kuendelea kuilinda misitu isiharibiwe.
Wito huo ameutoa wakati akizindua mkakati wa utekelezaji wa sera ya misitu ya (1998) na utiaji saini wa kanuni za uendelezaji wa nishati ya mkaa mbadala uliofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma.
Dk.Damas Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani humo amesema kuwa Watanzania hasa waishio mijini wakitumia mkaa mbadala basi misitu itaendelea kuwa salama na kuvifanya viumbe vinavyoishi kwenye misitu hiyo viendelee kuongezeka kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
Waziri huyo amesema kuwa hadi sasa hapa nchini wafanyabiashara 19 wameanzisha viwanda vya kuchakatia nishati ya mkaa mbadala hivyo kupitia kanuni zilizosainiwa zitawasaidia kupata uwezo wa masoko ndani na nje ya nchi hivyo kuifanya ajira iweze kuongezeka.
Kwa upande wake Kamishina wa Uhifadhi wa Wakala wa Huruma za Misitu (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema kuwa mkaa mbadala unapatikana kwa masalia ya miti na mabaki ya mimea mbalimbali ikiwemo mazao yanayolimwa na Wananchi.
Profesa Silayo amesema kuwa licha ya kulinda misitu lakini bado hata mwananchi ambaye ni mkulima bado atanufaika na mabaki ya mimea ya mazao yake kwa kuwa anaweza akayauza na kisha kumuingizia kipato cha fedha.
Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.Ezekiel Mwakalukwa amesema kuwa mkaa ni zao moja wapo linalotokana na mazao ya misitu hivyo utumiaji wa mkaa mbadala utawasaidia pia wananchi kutambua faida za matumizi ya mkaa huo.
Utiaji saini huo ambao umeenda sambamba na maadhimisho ya Majimaji selebuka ,umehudhuliwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali pamoja na baadhi ya wakazi wa mjini Songea ambao wengi wao wamedai wamenufaika na mpango huo wa matumizi ya nishati ya mkaa mbadala.