****************
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wazazi wenye Wanafunzi wamekubali kuwapeleka Watoto wao kwenye Mabweni kwa ajili ya kuweka kambi ya masomo kuanzia Jumatatu Agosti 5, 2019.
Hayo yamejili kwenye Mkutano Kati ya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu, Diwani Kata ya Miuta, Halmashauri za Serikali za Vijiji, uongozi wa shule na Wazazi wenye Watoto wanaosoma Madarasa ya mitihani kidato cha pili na cha nne wanaosoma Shule ya Sekondari ya Kitama II.
Wazazi hao ambao walielezwa umuhimu wa kuwekwa kambi za mitihani ni kwa ajili ya kuhakikisha Watoto wao wanapata muda wa kutosha wa kusoma na hivyo kuleta matokeo mazuri kwao kwenye mitihani ya Taifa.
“Tumefurahi kukaa kwa pamoja na kujadiliana na hatimaye tumekubaliana kwa pamoja tukiongozwa na Afisa Tarafa ambaye ametushawishi mpaka tukaelewa umuhimu, tunahaidi kuendelea kutoa ushirikiano na Watoto wetu tutawaleta kambini kwenye Mabweni ya shule.” alisema Ligwa Ahmad mojawapo ya Wazazi kikaoni.
Akizungumza kikaoni hapo Gavana Shilatu aliwashukuru Wazazi hao kuitikia wito na kukubali kwa azimio la pamoja lenye lengo la kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Nimekuja kuweka mwamko na kuwaonyesha Serikali ipo nanyi. Niwapongeze kwa kuunga mkono ombi la kuwaweka kambini Watoto wetu.” Alisema Gavana Shilatu
Shule ya Sekondari ya Kitama II ina bweni lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi 160 lakini wanaokaa bwenini hapo ni Wanafunzi 60 tu kwa sasa. Mara baada ya kikao Gavana Shilatu alienda kutembelea Mabweni hayo ambayo Wanafunzi wataweka kambi.
Kuwaweka kambini Madarasa ya Mitihani ni mojawapo ya mkakati wa kuongeza kiwango cha ufaulu kwenye Mitihani ya Kitaifa ndani ya Tarafa ya Mihambwe