Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya mashine ya kupulizia dawa za kudhibiti wadudu wadhurifu yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano Jijini Tanga.
Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akiongelea mkakati wa wizara hiyo wa kudhibiti mbu na wadudu wadhurifu ambao utatekelezwa nchi nzima, hapo ni katika makabidhiano ya mashine ya kupulizia dawa za kudhibiti wadudu wadhurifu yakiyofanyika katika viwanja vya Tangamano Jijini Tanga.
Viongozi wa Jiji la Tanga wakifurahia makabidhiano ya Mashine ya upuliziaji dawa za kudhibiti wadudu wadhurifu kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu. Makabidhiano hayo yalifanyika katika viwanja vya Tangamano jijini humo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (katikati), Mkurugenzi wa kinga wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Subi (wa kwanza kushoto) wakiwa pamoja na Mabwana Afya wa Jijini Tanga wanaotekeleza mkakati wa kudhibiti mbu na wadudu wadhurifu mkoani humo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapa na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Bw. Mustafa Mhina wakiangalia jinsi mashine ya upuliziaji inavyofanya kazi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa afya wa jiji la Tanga jinsi wanavyowanasa mbu kwa ajili ya kuwafanyia tafiti mbalimbali wakati wa hafla ya makabidhiano ya mashine ya upuliziaji dawa za kuangamiza wadudu wadhurifu iliyofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga.
*********
Na Emmanuel Malegi-WAJMW, Tanga
Jiji la Tanga limekua la pili kupata mashine za kupulizia dawa za kuua mbu na wadudu wadhurifu waenezao magonjwa mbalimbali ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI katika kudhibiti wadudu hao.
Akikabidhi mashine hiyo kwa uongozi wa Jiji la Tanga, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema mkakati huo ni wa miaka mitano (2019-2024) na unalenga kuhakikisha mbu na wadudu wadhurifu wanadhibitiwa kwa njia ya utengamano na ameiomba jamii ishiriki kikamilifu katika kupambana na wadudu hao.
“Wizara yangu imeagiza mashine nane za kisasa(foggig mashine) zenye uwezo mkubwa wa kupulizia na zinabebwa na magari na kupuliza eneo kubwa kwa wakati mmoja, hivyo naomba jamii ihakikishe inashiriki kikamilifu katika kupambana na wadudu hawa dhurifu”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa ni vema mikoa ikawekeza katika maeneo ya msingi am bayo ni pamoja na ushiriki wa jamii, sekta binafsi na wadau kushiriki katika kudhibiti wadudu kwa njia shirikishi zinazolenga kuharibu mazalia ya wadudu. Mikoa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa mbu na wadudu wadhurifu katika ngazi zote na kupanga njia madhubuti za udhibiti wa wadudu hao.
Waziri Ummy amesema katika kuhakikisha mkakati huu unatekelezwa, Wizara ya afya kwa kushirikiana na TAMISEMI imetoa maagizo kwa kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote ziweze kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ya utekelezaji wa udhibiti wa mbu na wadudu wadhurifu ambayo itakua mtaa kwa mtaa, Halmashauri kuhakikisha zinaishirikisha jamii katika ngazi zote za mapambano haya ya mbu na wadudu wadhurifu.
Pia Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kufanya tathmini ya utekelezaji wa mkakati huu katika kipindi cha mwaka mmoja na kutoa taarifa ya mafanikio, changamoto na mipango ya Halmashauri katika utekelezaji ikiwa ni pamoja na kununua mashine za upuliziaji (Fogging Machine) angalau moja katika kipindi cha kufikia Januari 2020.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga ambae ni Kaimu Mkuu wa Mkoa Bw. Thobias Mwilapa amemshukuru Waziri Ummy na Wizara ya Afya kwa ujumla kwa kuupatia mkoa huo mashine hiyo ambayo itasaidia katika utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti mbu na wadudu wadhurifu ambao wanaeneza magonjwa huku akiitaja Tanga kushika namba mbili kitaifa kwa ugonjwa wa Homa ya Dengue baada ya Dar Es Salaam.