Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Masala akizungumza na wananchi wa kata ya Bugogwa katika mkutano wa hadhara kwaajili ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili Ili kuzipatia ufumbuzi
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akizungumza na viongozi wa kata ya Bugogwa mtaa wa Igogwe inapojengwa shule tarajali ya sekondari kupunguza changamoto ya kufata elimu katika umbali mrefu
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala akiruka ukuta eneo la mwalo kata ya Bugogwa alipokwenda kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo
…………………………………………………………
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Elias Masalla ameridhishwa na nidhamu ya matumizi ya fedha za Umma katika ujenzi wa shule tarajali ya sekondari inayoendelea kujengwa mtaa wa Igogwe kata ya Bugogwa itakayosaidia kupunguza kero ya kufata elimu katika umbali mrefu na tatizo la mimba za utotoni.
Mhe Masalla amebainisha hayo wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kutembelea kata zote kumi na tisa zilizopo ndani ya wilaya hiyo kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi na kuzipatia ufumbuzi akiwa ameambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya, wawakilishi wa mamlaka ya Maji safi na salama jijini Mwanza MWAUWASA, shirika la umeme nchini TANESCO, mamlaka ya vitambulisho vya Taifa NIDA, Wakala wa Barabara za mijini na vijijini TARULA na wakuu wa idara za manispaa ya Ilemela ambapo amewapongeza wananchi na viongozi wa kata ya Bugogwa Kwa namna walivyojitoa na kutanguliza uadirifu katika ujenzi wa shule hiyo mpya Kwa kutumia gharama ndogo za ujenzi katika kukamilisha madarasa manne na ofisi Moja ya walimu
‘.. Kifupi niwapongeze, kujenga vyumba vinne na cha tano ofisi kwa gharama ya milioni ishirini maana sehemu nyengine unakuta hiyo milioni ishirini inajenga darasa moja tu ..’ Alisema
Aidha Mhe Masalla akawataka wananchi wa kata hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo sanjari na kudumisha amani na usalama huku akisisitiza kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 Kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Shukran Kyando ameahidi kuwa atashirikiana na uongozi wa kata ya Bugogwa na wananchi wake kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati Ili iweze kupokea wanafunzi Kwa mwaka ujao
Joachim Masanja ni miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano huo ambapo ameshukuru na kumpongeza Mkuu huyo wa wilaya Kwa kujitoa kwake katika kusikiliza kero za wananchi huku akishauri viongozi wengine na wataalamu kuacha kukaa ofisini badala yake wawafate wananchi walipo kutatua kero zinazowakabili.