Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba akifungua Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga.
Sehemu ya washiriki Wizara za kisekta, Idara za Serikali Wadau wa Maendeleo binafsi, Taasisi za Utafiiti na Elimu pamoja na Asasi za kiraia wakifuatilia Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021
Mkurugenzi Msaidzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Catherine Bamwenzake akizungumza wakati wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti (REPOA), Dkt. Donald Mmari akizungumza wakati wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma.
Afisa Mazingira Mwandamizi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Issa Nyashilu akitoa mada wakati wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padri Dkt. Charles Kitima akichangia wakati wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma.
Mdau wa Mazingira, Bi. Winnifrida Shonde akichangia wakati wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) Julai 23, 2021 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
……………………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga amesema Tanzania imekamilisha rasimu ya Mchango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contributions -NDCs).
Bi. Maganga amesema hayo Julai 23, 2021 jijini Dodoma katika hotuba ya ufunguzi wa Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba.
Alisema kuwa mchango wa NDC umetokana na Mpango wa Ahadi za Kitaifa (Intended Nationally Determined Contributions-INDCs) za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi uliowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Septemba 2015.
“Kama mnavyofahamu, nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na uwezo mdogo kifedha na kiteknolojia wa kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Kutokana na ukweli huo kuhimili mabadiliko ya tabianchi ndio kipaumbele cha nchi hizi,” alisema.
Bi. Maganga aliongeza kuwa nchi zinazoendelea kutokana na kutokuwa na viwanda vingi, hazijachangia au zimechangia kidogo katika uzalishaji wa gesijoto ambazo zinasababisha au zimesababisha mabadiliko ya tabianchi lakini kwa muktadha wa Makubaliano ya Paris nchi hizi zinatakiwa kutoa mchango katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na upunguzaji wa gesijoto kwa kuzingatia hali halisi ya nchi na uwezo wa kiuchumi kwa maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa Makubaliano ya Paris, kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto.
Akizungumzia Rasimu ya NDC alisema kuwa imeainisha hatua za kuchukuliwa kwenye eneo la kuhimili athari na pia kupunguza uzalishalishaji wa gesijoto na katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta za Kilimo, Mifugo, Misitu, Nishati, Mazingira ya Pwani na Bahari na Uvuvi, Rasilimali za Maji, Utalii, Makazi ya Binadamu, Afya, Miundombinu, na Upunguzaji Majanga.
Alisema shabaha ni kupunguza vihatarishi vya majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano sekta ya maji inatarajia kuongeza upatikananji wa maji safi na salama mjini na vijijini kutokaasilimia 60 hadi 90 ifikapo mwaka 2030.
Ili kuchangia katika upunguzaji wa gesijoto, shabaha ni kupunguza uzalishaji gesijoto kutegemeana na uwezo kiuchumi kuanzia asilimia 10 hadi 20 ya uzalishaji wa gesijoto nchini. Sekta za kipaumbele zitakazohusika na upunguzaji uzalishaji gesijoto ni nishati, usafirishaji, misitu na taka. Sekta hizi ndiyo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa gesijoto kwa sasa na zina fursa kubwa ya kuchochea na kuchangia maendeeleo ya kiuchumi .
“Suala muhimu la kutambua ni kuwa michango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi iliyobainishwa katika NDCs itatekelezwa kwa kuzingatia Kanuni ambazo NDCs imeweka. Kanuni hizo ni kuwa utekelezaji wa NDCs utategemea upatikanaji wa fedha na teknolojia kutoka Jumuiya ya Kimataifa na mifuko ya Kimataifa inayofadhili masuala ya mabadiliko ya tabianch,” alisisitiza.
Mpango wa Utekelezaji wa NDC umeandaliwa ukibainisha kwa kina shughuli zitakazotekelezwa kwa kila kusudio lililoainisha katika NDC na kiasi cha fedha kitakachohitajika. Kulingana na Mpango wa Utekelezaji wa NDC ulioandaliwa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 14,071,670,000 zitahitajika kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020.
Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa NDC zinategemea zaidi Mifuko ya Fedha iliyo chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na vyanzo vingine kimataifa. Ofisi zenye dhamana ya mazingira kwa Tanzania Bara na Visiwani yaani Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar zitafanya kazi kwa pamoja na sekta husika kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa katika NDC.
Kongamano hilo lilihusisha Wadau kutoka Wizara za kisekta, Idara za Serikali Wadau wa Maendeleo binafsi, Taasisi za Utafiiti na Elimu pamoja na Asasi za kiraia.