Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke Mhe. Suzan Kihawa (aliyenyoosha mkono) akifungua mafunzo ya kampeni ya Haki Mirathi, Wajibu Wangu kwa Viongozi wa ngazi mbalimbali wapatao 282 wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Temeke Jijini Dar es salaam Julai 22, 2021
Baadhi ya Viongozi wa ngazi mbalimbali wapatao 282 wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Temeke Jijini Dar es salaam walioshiriki mafunzo hayo ya Haki Mirathi wajibu wangu
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Temeke Mhe. John Ngeka akawakumbusha wajumbe wa mafunzo hayo kuwa Mirathi ni mchakato unaojumuisha kuwasilisha ombi la kuteua msimamizi wa mirathi mahakamani,
Baadhi ya Viongozi wa ngazi mbalimbali wapatao 282 wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Temeke Jijini Dar es salaam walioshiriki mafunzo hayo ya Haki Mirathi wajibu wangu
Afisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Joseph Mwakatobe akiwaasa washiriki kuwa migogoro mingi inayoigumbika mirathi mingi kwenye jamii ni kutokana na marehemu kuacha mali.
Moja ya mshiriki wa mafunzo ya Haki Mirathi Wajibu Wangu akiuliza swali.
Mtaalum Kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) akijibu maswali ya washiriki walioshiriki kwenye kampeni ya Haki Mirathi Wajibu Wangu
Moja ya mshiriki wa mafunzo ya Haki Mirathi Wajibu Wangu akiuliza swali.
*******************
Na Innocent Kansha – Mahakama
Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kushirikiana na wadau kutoka katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Chama cha Wanansheria Tanganyika (TLS) wamefanikiwa kuendesha na kutoa elimu ya Haki Mirathi Wajibu Wangu kwa Viongozi wa ngazi mbalimbali wapatao 282 wa Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Temeke Jijini Dar es salaam
Akifungua kampeni hiyo ya siku moja kwa viongozi hao mnamo Julai 22, 2021 na kufanyika katika ukumbi wa New Taifa Pub iliyoko Manispaa ya Temeke, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke Mhe. Suzan Kihawa aliwakumbusha wajumbe hao kuwa tatizo la mirathi ilimekuwa likiisumbua jamii kubwa kutokana na changamoto ya watu wengi kutokuwa na elimu ya kutosha ya namna ya kusimamia utaratibu mzima hasa pale inapotokea kifo.
“Tumeamua kwa dhati kwa kushirikiana na wadau kuanzisha kampeni hii ya haki mirathi kwa Wilaya ya Temeke kwani uzoefu unaonesha kwamba ukosefu wa elimu ya masuala ya mirathi miongoni mwa wanajamii ni mkubwa ikilinganishwa na migogoro mingi tunayoipokea na kuitolea maamuzi mahakamani”, alisisitiza Mhe.Kihawa
Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alisema uelewa wa mambo ya mirathi na wosia utakuwa chachu ya kuwaleta wadau wote kwa pamoja na hatimaye kupunguza migogoro katika eneo hilo muhimu. Jambo lolote likifanyika kwa wakati linaleta matunda yaliyokusudiwa na likicheleweshwa linazalisha hasara.
Mhe. Kihawa aliongeza kuwa, elimu hiyo ikipatikana kwa wakati itasaidia kutatua migogoro isiyo ya lazima kwa jamii. Aidha watu wasipokuwa na uelewa wananchelewa kufahamu haki zao, hivyo wanachelewa kuzitafuta na kupelekea kuchelewa kuzipata.
“Tunategemea baada ya mafunzo haya, mkawe mbegu njema katika mashina mnayofanya kazi, kusaidia watu kujua na kufuatilia haki zao kwa wakati hasa katika eneo la mirathi”, aliongeza Mfawidhi huyo
Mashauri yakifunguliwa kwa wakati ni wajibu wa Mahakama kuyasikiliza kwa wakati na wasimamizi wa Mirathi watekeleze wajibu wao wa kufunga hesabu za mirathi husika kwa wakati na hivyo kutimiza malengo ya kauli mbiu ya Haki Mirathi, Wajibu Wangu, alifafanua Mhe. Kihawa.
Naye, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Temeke Mhe. John Ngeka akawakumbusha wajumbe wa mafunzo hayo kuwa Mirathi ni mchakato unaojumuisha kuwasilisha ombi la kuteua msimamizi wa mirathi mahakamani, uteuzi wa msimamizi wa mirathi ambaye atakuwa na majukumu ya kukusanya mali za marehemu, kulipa madeni kama yapo pia kulipwa madeni kama itathibitika marehemu alikuwa akidai na hatimaye kugawanya mali za marehemu kwa warithi.
Mhe. Ngeka aliongeza kuwa Sheria zinazosimamia mirathi hapa nchini (sheria ya Serikali, sheria ya Mila na sheria ya Kiislamu) zinatamka kuwa mtu yoyote ili mradi asiwe chini ya miaka 18, mwenye uaminifu na uadilifu anafaa kuwa msimamizi wa mirathi bila kujali kuwa ni ndugu wa marehemu au la.
Mhe. Ngeka aliendelea kusema, kwa utaratibu uliopo baraza la ukoo ndio huteua msimamizi wa mirathi ambaye baadae anathibitishwa na Mahakama, lakini iwapo baraza la ukoo likashindwa kumteua msimamizi kwa kushindwa kuafikiana katika kikao basi mtu yoyote anaweza kwenda mahakamani kuomba kuteuliwa na Mahakama kuwa msimamizi wa mirathi husika.
Wakati huo huo, Afisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Joseph Mwakatobe aliwaasa washiriki kuwa migogoro mingi inayoigumbika mirathi mingi kwenye jamii ni kutokana na marehemu kuacha mali na njia bora ya kuondokana migogoro huyo ni kuandika Wosia wenye kukidhi vigezo vyote usioweza kupingika hata mahakamani.
“Usipo andika wosia unajiondolea au kupoteza nguvu na mamlaka ya kisheria ya mali zako zote ulizochuma ili zisaidie familia yako, wosia utasaidia kutofuja mali za marehemu na hivyo warithi kunufaika bila kuingia kwenye mgogoro wa aina yoyote”, alifafanua Afisa huyo kutoka RITA.