***************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera, amewaagiza wakuu wa idara ya elimu, kuandaa na kuweka mpango mkakati wa kupunguza na kukabiliana na tatizo la utoro na mimba za utotoni kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.
Dk Serera amesema baadhi ya wanafunzi wa kike wamekuwa wakikatisha masomo yao kutokana na kupata ujauzito na wengi kushindwa kuhudhuria masomo baada ya kubebeshwa mimba bado wakiwa wanasoma.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri hiyo, wakiwasilisha mpango mkakati na bajeti ya idara na vitengo hivyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
“Wakuu wa idara za elimu mnapaswa kuweka mpango mkakati ambao utatekelezeka ili kupunguza na kuondoa tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi,” amesema Dk Serera.
Ametoa rai kwa wataalamu hao wa idara ya elimu, kuwashirikisha wazawa waliopata fursa ya kupata elimu, kushawishi wazazi na walezi wa eneo hilo, kuwapeleka watoto wao shule na kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria masomo kwa vipindi vyote vya muhula wa masomo na kuimarisha mfumo wa elimu kwa watu wazima (MEMKWA).
Hata hivyo, amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Yefred Myenzi, kuanzisha karakana maalumu ili kupunguza gharama za utengenezaji wa madawati na ukarabati wa madawati chakavu.
Pia, amewaagiza maofisa elimu ngazi ya wilaya na waratibu wa elimu kata, kutoa taarifa za ufundishaji na mahudhurio ya walimu shuleni na walimu kumaliza mitaala ya masomo kwa wakati ili kutoa muda kwa wanafunzi kujiaanda na mitihani mbalimbali.
Amemuagiza mganga mkuu wa halmashauri hiyo kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati katika zahanati, vituo vya afya, hospitali na ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za afya na ukusanyaji wa mapato kupitia mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa (iCHF).
Amewataka wataalamu wa afya kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa (iCHF), kwa wananchi ili kuimarisha mfuko huo ili uweze kuhudumia wananchi kwa gharama nafuu.