Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa tatu kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro (wa tatu kulia) wakati akikagua maendeleo ya kivuko cha MV. MAFANIKIO ambacho kimeletwa katika yadi ya Songoro Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro (wa pili kulia) na Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana kulia wakikagua kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro akimuonyesha kitu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle wakati akikagua kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma. Kulia ni Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akimuonyesha kitu Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro kulia wakati wakikagua moja ya milango ya kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma. Katikati ni Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA DAR ES SALAAM)
*****************************
Huduma za Kivuko kwa wakazi wa Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara zinatarajiwa kurejea baaada ya takribani wiki tatu kutoka sasa, hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle leo wakati alipotembelea eneo la Yadi ya Songoro Marine Kigamboni jijini Dar es Salaam kukagua maendeleo ya ukarabati huo unaofanywa na kampuni ya Songoro.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua ukarabati wa kivuko hicho, Mtendaji Mkuu Maselle amesema kivuko hicho kipo mbioni kukamilika kwani Mkandarasi ametakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda mfupi ili wakazi wanaotegemea kivuko hicho Mkoani Mtwara waweze kurejeshewa huduma zake mapema iwezekanavyo.
‘’Tumekisafirisha kivuko hiki kutoka Mtwara kuja hapa Dar es salaam kwakuwa ni gharama ndogo kukileta hapa kuliko kusafirisha vifaaa vyote vya matengenezo kwenda kufanyia Mtwara ndio maana mkandarasi akaamua kukivuta kivuko hiki kije hapa ili muda wa matengenezo uwe mfupi zaidi’’.
Mhandisi Maselle amesisitiza kuwa utaratibu wa kufanya matengenezo kwa vivuko vya TEMESA ni muhimu sana kwa vyombo vya maji kwakuwa maji ya bahari yana chumvi nyingi na kali hivo kama kivuko kitakuwa hakijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kitakuwa kinaharibika na kitashindwa kufanya kazi kwani chuma chake kitaliwa na maji ya chumvi na hivyo kushindwa kudumu kwa muda mrefu.
‘’Ni utaratibu wa kawaida kwa TEMESA kila ambapo kivuko kinafikia muda wake wa matengenezo kinga, lazima kitolewe na kupelekwa kufanyiwa ukarabati na matengenezo na hii ni hatua mojawapo ambayo tumefanya na tunaendelea na ukarabati wa vivuko vingine ambavyo muda wake wa ukarabati umefika’’. Alisema Mhandisi Maselle ambapo amewaomba wakazi wa Mtwara wavumilie wakati kivuko hicho kikiendelea kufanyiwa ukarabati ambapo wakazi hao wamepelekewa boti mbili za MV. TANGAZO na MV. KUCHELE ambazo zinatoa huduma kwa sasa kwa wakazi hao.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo la ukaguzi amesema, ukarabati wa kivuko hicho umefikia asilimia 85% na ameongeza kuwa wanatarajiwa kumaliza ukarabati wake ifikapo Tarehe 15 mwezi Agosti.
‘’Kazi kubwa zote tulizozifanya ziko kwenye hatua ya mwisho ili kuweza kukamilisha ukarabati wa kivuko hicho,’’ amesema Songoro.
Kivuko cha MV. MAFANIKIO kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50 na kinatoa huduma zake kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara mjini.