NA MWANDISHI WETU, SENGEREMA
MRADI wa uanzishwaji wa Kituo kitakachosaidia kuondoa changamoto
zinazoikabili jamii nchini hususan maeneo ya vijijini, umetambulishwa kwa
wananchi wilayani Sengerema mkoani Mwanza na Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe.
Erick Shigongo.
Mradi huo utakaokuwa chini ya Taasisi ya “Kijiji” utatekelezwa katika Kijiji cha Kasisa jimbo la Buchosa, Wilayani Sengerema
Mkoani Mwanza, umebuniwa na Familia ya Aliyekuwa Mbunge wa Kwanza wa
Kuchaguliwa jimbo la Sengerema kati ya mwaka 1965-1985, marehemu Alphonce
Rulegura, ili kuenzi nia yake njema ya kuwawezesha wananchi wa jimbo hilo
kuondokana na umasikini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi hiyo mjini
Sengerema, Mbunge wa jimbo la Buchosa ambalo liko wilayani humo, Mhe. Erick
Shigongo alisema, mradi huo utaleta faida kubwa sio tu kwa wanakijiji wa Kasisa
na maeneo jirani lakini pia nje ya jimbo la Buchosa.
“ Kilichofanyika hapa leo hii ni baraka kubwa sana na nina uhakika
marehemu Rulegura huko aliko mbinguni ana furaha kubwa sana kwani jambo hili
linaendeleza mema aliyokuwa akiyafanya kwa watu wa Sengerema,” alisema Mhe.
Shigongo
Alimpongeza Muasisi na Rais wa Taasisi hiyo ya “Kijiji”, Bi. Clara
Luregura Ford, ambaye ni binti wa marehemu Rulegura kwa kuona umuhimu wa
kuendeleza ndoto za marehemu baba yake licha ya kwamba kwa sasa binti huyo
anaishi na kufanya kazi nchini Marekani.
“Ninachokishuhudia hapa leo ni fundisho kuwa watoto tunao wajibu
wa kuziishi na kutimiza ndoto za wazazi wetu na kuhakikisha majina yao
hayapotei kwa sisi kutenda mambo mema katika jamii tunazoishi.” Alisema Mhe.
Shigongo.
Akielezea malengo ya Taasisi ya “Kijiji”, mjumbe wa Bodi,
Bw. Martin Rulegura alisema ni kuchagiza swala la maendeleo endelevu
katika Tanzania kupitia elimu, uwezeshaji wa jamii, wanawake na vijana.
Alisema
wazo la kuanzishwa taasisi ya Kijiji lilianza mwaka 2018 wakati Muasisi na Rais
wa Taasisi hiyo, Bi. Clara Rulegura Ford akiongozana na familia yake
alitembelea kijiji cha Kasisa, mahala alikozaliwa baba yake na kwamba
alipokelewa kwa furaha na wana kijiji ambao walimueleza changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo.
“Mlinipatia risala ya mahitaji na nikaahidi ninavyoweza kusaidia
na ilinichukua miaka mitatu baada ya kufanya utafiti kufikia uamuzi huu, lengo
langu halikuwa kutoa fedha tu, na sasa tumefika mahala ambapo tunaweza kuanza
kushughulikia changamoto zetu.” Alisema Bw. Martin akinukuu hotuba ya Muasisi
na Rais wa Taasisi ya Kijiji Bi. Clara Rulegura Ford.
Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi na watu werevu na kama
alivyosema baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kwamba Watu Tunao na Ardhi tunayo
hakuna sababu ya maana wananachi washindwe kuishi maisha yao kwenye uhuru wa
Kiuchumi.
Hivyo ili kutatua tatizo la umasikini ni lazima kujua asili yake
ili kuung’oa umasikini kutoka kwenye mizizi yake, Alisema Bi. Clara kwenye
hotuba hiyo.
“Ndio maana hiki Kituo kitajikita katika miradi 9 ambayo ni kutoa
elimu ya mafunzo ya ufundi stadi, Nyumba endelevu na imara, Ufanisi
wa Nishati, Nishati Mbadala, kujenga miundombinu wezeshi ya Upatikanaji
wa maji safi na salama, Usanifu wa vyoo na mifumo ya majitaka, elimu ya Afya,
Kilimo endelevu na cha Umwagiliaji, Udhibiti wa taka na uchakataji.”
Alifafanua Bw. Martin.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, ambaye aliwakilishwa na Afisa
Tarafa wa Wilaya hiyo Bw. Fadhili Abel alisema kwa niaba ya Serikali na
wananchi wa Sengerema wanaipongeza Taasisi ya Kijiji kwa kuja na mradi huo
kwani utaharakisha nia ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
“ Safari ya kuwaletea maendeleo wananchi ambayo serikali
ingechukua miaka 50, lakini tukiungana na Taasisi zisizo za Kiserikali kama hii
ya Kijiji tunaweza kuchukua miaka 10 tu kuwafikisha wananchi wetu katika maisha
ambayo wanastahili kuishi.” Alibainisha Bw. Fadhili.
“ Jukumu mnalolitekeleza linarahisisha utendaji kazi wa Serikali,
changamoto zitakazoenda kutatuliwa na hii Taasisi ya Kijiji, kwa namna moja au
nyingine itarahisisha maendeleo ya watu wetu huko katika kijiji cha Kasisa na
sio Kasisa pekee lakini pia maeneo mengine nje ya kijiji.” Alifafanua na
kuongeza…..Pale ambapo viongozi wa Taasisi wanapohitaji msaada wa Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya iko wazi kusaidia.
Kwa upande wao, wanakijiji wa Kasisa ambako ndiko kutajengwa Kituo
hicho wameeleza furaha yao na kutaja vipaumbele vyao kuwa wangependa Taasisi ya
Kijiji ianze kutatua shida ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama ikifuatiwa na
eneo la Elimu kwa na Afya.
“ Tunaomba mradi uanze na maji, tunasumbuka na maji, maji yetu sio
salama, tunapata maji kutoka ziwani na kisimani, ziwani ni mbali na haya ya
kisimani ni machafu na tunatumia kwa kupikia na kunywa.” Alisema Bi. Sabina
Paulo, ambaye ni anatoka kitongoji cha Kigongo.
Alisema maji ya kutumia kwa kunywa na kupikia wanayapata kutoka
ziwani na visimani.
Hata hivyo ili upate maji ya ziwani unatembea umbali mrefu wakati
yale ya kisimani hayana ubora unaotakiwa na hivyo amesisitiza kuwa mradi uanze
na kutatua changamoto ya Maji na mingine itaendelea kufanyiwa kazi.
“Mimi ninafurahia mradi huu, mimi ni fundi wa kuchana mbao kwa
kutumia mikono na msumeno, nimeshazeeka, watoto wangu wakipata elimu ya ufundi
kutumia mashine za kisasa itasaidia katika kazi zetu.” Alisema mwanakijiji
mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Makoye Shilole Shigemelo.
Katika uzunduzi huo Familia ya Marehemu Rulegura iliongozwa na
Mkewe, Bi. Margaret Rulegura na watoto wake Coleta Mnyamani na Martin
Rulegura.
Mbunge wa jimbo la Buchosa Mkoani Mwanza, Mhe. Erick
Shigongo (kulia) akisalimiana na Bi. Margaret Rulegura, Mjane wa aliyekuwa
Mbunge wa kwanza wa jimbo la Sengerema kuanzia 1965-1985, Marehemu Alphonce
Rulegura huku Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Kijiji, Bw. Martin Rulegura
(katikati) akishuhudia, wakati Bw. Shigongo alipofika kuzindua taasisi hiyo
mjni Sengerema juzi. Taasisi hiyo itajenga Kituo cha kutoa elimu ili kuchagiza swala la maendeleo endelevu katika Tanzania kupitia elimu,
uwezeshaji wa jamii, wanawake na vijana.
Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya KIJIJI, Bw. Martin Rulegura, akitoa hotuba kwa niaba ya Muasisi na Rais wa Taasisi hiyo, Bi. Clara Rulegura Ford.