Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akila chakula cha wafungwa katika Gereza la Kilimo na Mifugo la Isupilo, Wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa, wakati alipofanya ziara gerezani hapo,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia), akimvalisha Koti la Polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Juma Bwire, alipotembelea Kituo cha Polisi Mafinga, Wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akikagua pikpiki katika Kituo cha Polisi Kilolo, wakati alipokitembelea Kituo hicho Kikuu cha Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia), akikaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga ofisini kwake baada ya kumaliza ziara ya siku mbili Mkoani humo,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akisalimiana na Wawekezaji wa Viwanda mbalimbali Wilayani Mufindi, wakati alipokuwa anawasili Kiwanda cha Hongwei, Mjini Mafinga, Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuzungumza na wawekezaji hao kutoka China.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akisonga ugali wa Wafungwa katika Gereza la Iringa wakati alipofanya ziara katika Gereza hilo
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akiangalia Mpaka wa Jeshi la Magereza na Mkazi wa Mafinga wakati alipofika Mjini Mafinga Julai 20, 2021, kutatua mgogoro wa mpaka huo uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
………………………………………………………………
Na Felix Mwagara, MOHA-Dodoma.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi Mkoani Iringa, anatarajia kuanza ziara ya siku tano katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ya kukagua miradi mbalimbali pamoja na utendaji kazi wa Taasisi zake katika Mikoa hiyo.
Waziri huyo anatarajia kuanza ziara hiyo Julai 22 hadi 27, 2021 ambapo ataambatana na Wakuu wa Taasisi wa Wizara yake katika Mikoa hiyo katika siku zote atakazofanya ziara.
Akizungumza na Mwandishi wa Habari hii, Waziri Simbachawene amesema, amemaliza salama ziara yake katika Mkoa wa Iringa, ambapo amezipongeza Taasisi zake ambazo ni Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mkoani humo kwa kuwa na umoja pamoja na kufanyakazi kwa weledi.
“Lengo kuu la ziara yangu ni kuona utendaji kazi wa hizi Taasisi zangu na pia kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali katika Mikoa hiyo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitatua, na pia kuwasisitiza utendaji kazi wa haki kwa kuwajali na kuwasikiliza wananchi wanapopatwa na matatizo mbalimbali wakihitaji huduma kutoka kwenye Taasisi hizo,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, anatarajia kuwasili Mkoani Kilimanjaro Julai 22, 2021 na katika Mkoa huo baada ya kufanya Kikao na Mkuu wa Mkoa huo, atakagua shughuli za kiutendaji katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP), Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda Moshi (TRITA) na baadaye atazungumza na Wakuu wa Taasisi zote zilizopo ndani ya Wizara yake katika Mkoa huo.
Katika ziara ya Mkoa wa Arusha, Waziri huyo amefafanua kuwa, Julai 24, 2021 ataanza ziara Mkoani humo kwa kutembelea Makao Makuu ya Taasisi zake na kuangalia utendaji kazi wao pamoja na kukagua miradi iliyopo katika Mkoa huo.
“Ziara yangu ya Iringa, na pia hii ya Kilimanjaro na Arusha inanisaidia kujua mengi kuhusu hizi Taasisi zangu na pia kujua mafanikio yao pamoja na changamoto walizonazo, ambapo ndani ya Mkoa wa Arusha pia nitafika Mpaka wa Namanga kwa ajili ya kukagua Mpaka huo pamoja na shughuli za kiutendaji za Uhamiaji Mpakani hapo,” alisema Simbachawene.
Waziri Simbachawene anatarajia kumaliza ziara yake Julai 27, 2021 na atarejea ofisini kwake jijini Dodoma kuendelea na shughuli za kiofisi.