**************************
Na WAMJW – Mbeya
Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha zote zilizobakia na kufanya jumla ya Bilioni 9.2 kukamilisha Ujenzi wa jengo la ghorofa sita kwa ajili ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wazazi META, mkoani hapa.
Jengo Hilo ambalo limekamilika kwa asilimia 85, linatarajiwa kuanza kutoa huduma kabla ya kumalizika mwezi Oktoba mwaka huu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amefanya ziara ya dharura kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya afya inayoendelea mkoani humo.
Akizungumza, Waziri Gwajima amesema amefurahi kuona maendeleo mazuri ya ujenzi huo wa jengo hilo, litakapokamilika litasaidia kuimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto.
“Mh. Rais Samia Suluhu Hassan ameshamalizia kutoa fedha zote na kufanya jumla ya Sh. bilioni 9.2 za ujenzi huu hii ni kwa kuwa anajali katika vipaumbele vinavyopunguza Kero kwenye huduma za afya hususan kero za huduma wazazi na watoto wachanga wakati wa kujifungua.
“mradi huu utakapokamilika idadi ya vitanda itaongezeka kutoka 150 hadi 400, ni jengo kubwa lenye ghorofa kama sita, limejengwa maridadi sana, lina vyumba vya kutosha na vitanda vya kujifungulia vya kutosha na vyumba vya upasuaji,” amesema.
Dkt. Gwajima ameongeza “Tumesema wajitahidi wafanye kazi usiku na mchana (kumalizia ujenzi) kufikia mwezi wa 10 wawe wamemaliza kufanya hii kazi.
Wakati huo huo, Waziri Gwajima amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa wodi kwa ajili ya watu wanaohitaji kufanyiwa upasuaji linalojengwa pamoja na vyumba sita vya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
“Jengo litakuwa na vitanda 82 vitakavyolaza watu waliofanyiwa upasuaji au wanaosubiri kufanyiwa upasuaji na hii ni hatua kubwa sana kuwa na vyumba vya upasuaji sita.
“Hii ni hatua kubwa sana ambayo mpaka sasa mmeshapewa hizo bilioni 3 na mnapiga hesabu kuweza kumalizia hiyo kazi iliyobaki,” amesema.
Ameagiza viongozi wa Mkoa huo kujitahidi kulimaliza mapema lisivuke mwaka huu mwezi wa nane liwe limeanza kutoa huduma.
“Mmekadiria Bilioni 5.5, fanyeni haraka hizo hesabu zije ili muweze kupewa hizo fedha hatutaki kumaliza mwaka huu hamjaanza kufanya kazi ya upasuaji kwenye haya majengo.
“Muwapunguzie pia mzigo Hospitali ya Rufaa ya Kanda kwa kuwahudumia wagonjwa wengi ambao mngeweza kuwaona ninyi pasipo ulazima wa rufaa.
“Nimefarijika kuona pia jengo la masuala yote yanayohusika na huduma za dharura kwa ufadhili wa Global Fund , limekamilika.
Ameongeza “Nimeona pia mitambo ya oksijeni iliyounganishwa na mtambo wa kufua oksijeni ambayo imesimikwa kwenye hospitali saba za mikoa na bado tunasubiri hospitali nyingine 12.
“Huu ni ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na wadau wake wakiwamo World Bank na Global Fund.
“Ndiyo maana tunasema nchi yetu inaendeshwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wanaoitakia mema Serikali hii na Mh. Samia anaendelea kuweka mazingira mazuri ili tupate wadau wengi wanaoweza kushirkiana na sisi.
“Kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa ‘force account’ hata wakija wakiangalia watafurahi, wataleta zaidi ushirikiano wa misaada mbalimbali katika kuboresha huduma za sekta ya afya,” amepongeza.
Amewataka kuhakikisha wanalikamilisha mapema ili lianze kutoa huduma na uzinduzi wa huduma ufanyike kabla ya Septemba.
“Nawapongeza mkoa na watumishi ambao mmekubali kuvumilia changamoto mbalimbali za stahiki zenu ili mpanue huduma, wateja wengi waje kisha muweze kunufaika na bima ya afya wanayotumia wengi kwa kuvutiwa na ubora wa huduma”.
“Bima ya afya sheria inakuja, Mungu akisaidia kuanzia mwakani hakutakuwa na mteja anayekuja wa msamaha, kazi iliyobaki kwenu ni huduma nzuri kwa wateja na tabasamu, maana mtu mwenye hela yake anaweza kuamua kwenda zake asitumie huduma yako iwapo haimridhishi hivyo utabaki huna wateja huku miundombinu unayo.
“Haya maslahi yetu tunayosema tunachelewa kulipwa tayari Serikali imetuwekea mtaji wa miundombinu, vifaa na utaalamu tushindane kwa ubora wa huduma ‘marketing’ ili tupate wateja wengi waliojiunga na bima za afya ili hatimaye kusiwe na kuelemewa na misamaha kwa kuwa wote watakuwa na bima za afya.
“Wakija wengi kwa sababu wanapata huduma hapa, nanyi mtapata mapato mengi ya hospitali yatokanayo na mfuko wa bima, na mkumbukrle kuwa mna kamati zenu, bodi zenu hivi atakayekuja kuwapangia ni nani, tabasamu lako hela yako, anzeni hizo sera.
“Hatuombei watu waumwe lakini tumeumbiwa magonjwa hata huko ulaya walikoendelea watu wanaumwa na wanajiunga na bima hasa mtu akishakuwa kwenye bima ndugu zangu tayari huo ni uwekezaji maana ile bima ni ya afya na watakuja kupata huduma na hela hiyo itaendeleza afya kwa ujumla wake.
“ Na wakifurahia zaidi watazidi kujiunga zaidi na ninyi mtafurahi kwa kutoa huduma yenu na kuwafanya watu bima zao zitumike kwenu, tunahesabu kama miezi mingine 18 hizi kelele zingine za extra duty, on call, dawa zitakuwa hazipo, zitakuwa zimepotea.
“Msipojifunza kuyapokea haya na kujituma kwa uadilifu tutajikuta tumeachwa tupo watumishi wengi, vifaa tunavyo lakini wateja hatuna wameenda kwenye huduma bora zaidi za wenye kutabasamu.
“Kwa sababu wawekezaji watatoka nje ya nchi na matabasamu yao watakuja kuwekeza huku huku mbeya kwenye huduma hiyo hiyo unayoitoa utajikuta wewe unaulizwa na Serikali nakulipa mshahara kwa kulinda majengo, mitambo na vifaa au kwa kutoa huduma, hilo ni swali ambalo litageuka kuwa la kwetu hivyo tutafute majibu lakini tukikaa mkao wa kusubiri bima ya afya kwa wote ije, tabasamu tunalo vifaa tunavyo tutafurahi,
“Watu wataelewa na magonjwa yatatoweka yatabaki ya kinga tu, tutachukua utaalamu wenu tuendelee na kinga zaidi ,” amesema Waziri Gwajima.
Awali, akizungumza, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt.Chuwa Chuwa amemuhakikishia Waziri Gwajima kwamba watahakikisha wanasimamia maelekezo aliyoyatoa.
“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa sisi kama Wilaya tunakushukuru sana kuja kufanya ziara katika Mkoa wetu, Watanzania wanakuona na tunafahamu namna ambavyo unahangaika kupigania afya za Watanzania tunakushukuru sana.
“kwa namna ya kipekee mwenyewe umeona na kukagua miradi ambayo ina karibu Sh. bilioni 14 ukijumlisha. Kwa kweli ni miradi mikubwa tunaomba upeleke salamu kwa Mh. Rais kazi yake aliyoifanya kwa mkoa wa Mbeya ni kubwa sana na wanambeya kiujumla wanaona namna ambavyo anahangaikia afya zao.
“Na sisi tukuahidi Mh. Waziri kwamba tutaendelea mara kwa mara hii miradi na tutaendelea kuisimamia kadri unavyotoa maelezo, hii ni mara yangu ya pili katika kipindi kifupi nilichokaa hapa, kutembelea kwenye hii miradi na mradi ambao tuliukagua kabla ya kufika hapa.
Amesema alishatoa maelekezo kwamba wafanye kazi usiku na mchana, nimemuona leo msimamizi kutoka TBA na ameniambia ameongeza muda wa kufanya kazi, muda si mrefu naamini watanzania wataanza kupata huduma kwenye miradi hii.