…………………………………………………………………………………..
Wazee Wilayani Busega kupatiwa Bima ya Afya (CHF) ili kuondoa kero ya matibabu kwa kundi hilo. Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria na wazee wa Wilaya ya Busega kilichofanyika Shule ya Msingi Nyashimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema tayari upo mpango wa kuwapatia Bima ya Afya wazee 14,000 ambapo ili kupunguza changamoto ya matibabu kwa wazee, wazee wapatao 6,000 wataanza kupatiwa Bima hizo.
Awali Akisoma taarifa ya Wazee, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Busega Bw. Kubagwa Madalia amesema wazee wanashiriki kwa ukaribu katika vikao mbalimbali vya maamuzi, ikiwemo vikao vya baraza la madiwani na vingine vinavyotambulika kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema yupo tayari kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wazee na kuahidi kwamba ataimarisha ulinzi na usalama kwa wazee na hakuna vitendo vitakavyohatarisha usalama wao. Pia Mhe. Zakaria amesema kwamba yupo tayari kushirikiana na wazee katika kukuza maendeleo na kuwataka wazee waliohudhuria kikao hicho kuwa mabalozi na kuzipeleka salam kwa wazee wote wilayani Busega.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ameanza utaratibu wa kuongea na makundi mbalimbali wilayani Busega ikiwa ni kujitambulisha kwa makundi hayo na ameanza na kundi la wazee.