Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka jengo na Msingi katika majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga-Kasulu, Kigoma. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na Balazi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Pamela O’donnel.
Walimu tarajali wa Chuo cha Ualimu Kabanga wakifurahia baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kuweka jiwe la msingi katika majengo mapya ya Chuo chao kilichopo Kasulu, Kigoma
Balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O’donnel akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga- Kasulu Mkoani Kigoma.
Muonekano wa jengo la madarasa mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga kilichopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma
Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo pamoja na Balozi wa Canada nchini Tanzania wakiwa wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa SUMA JKT ambao ndio wamejenga Majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga
********************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango amesema ujenzi wa majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga ni moja ya mikakati ya Serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu ya Nchini.
Ameyasema hayo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati wa kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa majengo mapya ya Chuo hicho ambapo amewataka walimu tarajali kusoma kwa bidii kwa kuwa sasa miundombinu imeboreshwa.
Kiongozi huyo amesema ameridhishwa na taarifa Ujenzi huo kwa kuwa umezingatia matumizi Bora ya Nishati mbadala na nafuu na pia uhifadhi wa mazingira. Aidha amesema ni vizuri chuo hicho kikachukua tahadhari zote za kuzuia majanga yakiwemo ya moto na kuwataka walimu tarajali wa Chuo cha Ualimu Kabanga watakaohamia katika majengo mapya ya Chuo hicho kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Pia ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuwezesha ujenzi wa majengo hayo mapya ya Chuo cha Ualimu na Vyuo vingine vya Ualimu nchini.
“Serikali ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan inathamini urafiki wa muda mrefu na ndugu zetu wa Canada, nakuomba Mhe. Balozi kupitia kwako utupelekee salamu zetu kwa Waziri Mkuu wa Canada kutoka kwa Watanzania, tunaishukuru serikali yake pamoja na wananchi kwa kuendelea kushirikiana nasi tunapofanya jitihada za kujikomboa kielimu na katika maeneo mengine ya nchi yetu Canada imekuwa mbia muhimu,” amesema Makamu wa Rais
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Mradi huo mpaka utakapokamilika utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 11 na kwamba umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Programu ya Kuimarisha Elimu ya Ualimu (TESP).
Ndalichako amesema mradi huo utakapokamilika utaongeza idadi ya Wanachuo kutoka 400 hadi 800 na utakuwa na miundo mbinu yote na vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Sekta ya Elimu, Serikali ya Canada imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali na kushirikiana nao kwenye masuala yanayohitaji ushauri wa kitaalamu hususani kwenye mambo ya elimu ya ualimu ambapo programu ya TESP ambayo ni ya Miaka 7 ina thamani ya jumla ya dola za Canada milioni 53 ambazo ni sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 90 za Tanzania.
Nae balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O’donnel amesema Canada inayofuraha kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika juhudi za kuboresha mfumo wa ufundishaji kwa faida ya watoto wa kitanzania
Amesema ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ni wa kisasa unaozingatia mbinu za kimazingira na hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kuchangia juhudi za Serikali za kukabiliana changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi. Pia itachangia jitihada za maendeleo endelevu ambayo ni nishati safi usawa wa kijinsi na kupambana na madiliko ya tabia nchi na hivyo kukifanya Chuo hicho kuwa cha karne.
Balozi O’dennel ameongeza Canada ni moja ya nchi ya kwanza duniani kupitisha sera ya nchi yenye kuzingatia usawa wa kijinsia na kwamba anafarijika kuona mradi unahakikisha wakufunzi wasimamizi wa elimu na mifumo yote inazingatia usawa wa kijinsia na kwamba Serikali yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha Sekta ya Elimu Hususan Elimu ya Ualimu.