Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea jezi ya timu ya taifa ya Morocco kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco Faouzi Lakjaa wakati alipotembelea eneo la Mchezo wa Mpira wa Miguu la Mohammed wa VI (Mohammed VI Football Complex) kuona uwekezaji wa miundombinu ya mpira wa miguu uliofanywa katika eneo hilo Nchini Morocco
………………………………………………………………………………….
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) litaendelea kuimarisha mahusiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco ili kukuza kiwango cha mpira huo nchini .
Amesema hayo jana (Alhamisi Julai 15, 2021) baada ya kutembelea Ofisi za Shirikisho hilo na eneo la Mchezo wa Mpira wa Miguu la Mohammed wa VI kuona uwekezaji wa miundombinu ya mpira wa miguu uliofanywa katika eneo hilo.
Amesema kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco liendelee kutumia fursa ya mafunzo kwa pande zote mbili lengo likiwa ni kuwa na timu za taifa zilizo bora na zenye ushindani kama ilivyo kwa timu ya taifa ya Morocco.
Aliongeza kuwa shirikisho hilo limekuwa likiisadia sana Tanzania katika kujifunza mbinu mbalimbali za kiutawala pamoja na mbinu za kimichezo kupitia timu za taifa za Tanzania.
“Timu zetu za taifa za Taifa Stars, Serengeti Boys, Ngorongoro na Twiga Stars zimekuwa zikija hapa Morocco kuweka kambi kwa gharama ya Serikali yao, hili ni jambo kubwa na la kuendeleza”
Kadhalika Waziri Mkuu alisema kuwa katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Morocco Saad Dine El Otmani alikumbushia ahadi ya Mfalme wa nchi hiyo juu ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Mohammed VI uliopangwa kujengwa jijini Dodoma “tumemkumbusha na ameahidi kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kumkumbusha mfalme ili ujenzi uanze kwa kuwa kila kitu kipo tayari”