*****************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge, amesema hatosita kumchukulia hatua kali ya kisheria yeyote yule atakaefanya uvamizi wa ardhi wa aina yeyote.
Alieleza hayo wakati wa kuzindua Kampeni ya kushughulikia Migogoro ya Sekta ya Ardhi Mkoani Pwani,uzinduzi uliofanyika Mjini Kibaha,uliomshirikisha William Lukuvi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Kamati ya Usalama ya Mkoa.
Alieleza kuwa watafanya ziara na Waziri wa Ardhi katika Wilaya za Kibaha, Bagamoyo, Mafia, Mkuranga, Rufiji na Kibiti kuanzia Tarehe 14 Julai,2021 hadi Tarehe 22 Julai 2021 kushughulikia na kutatua Migogoro ya Ardhi.
Kunenge, aliwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanatumia nafasi zao katika kutatua migogoro ya Ardhi.
Kunenge pia aliwataka Viongozi hao wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanaboresha Daftari la makazi na kuhakiki idadi ya mifungo iliyopo mkoani Pwani ili kuepukana na Migogoro ya Ardhi.
Naye Waziri Wa Ardhi Lukuvi kwa Upande wake amewataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanatatua migogoro ya Ardhi na wasisubiri mpaka wananchi waje kulalamika kwa Viongozi wakuu,
Aliziagiza Halmashauri zote Tanzania kuhakikisha wanazisimamia kampuni binafsi za upimaji wa ardhi na wasiziache zikafanya kazi zenyewe.
“Kampuni Binafsi lazima zisimamiwe na zisiachwe zifanye kazi zenyewe kwani msimamizi wa Ardhi katika Halmashauri ni Halmashauri” alisema Lukuvi.