Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL), limetoa mafunzo kwa wanawake na wanafunzi wa Kata ya Ikhanoda baada ya kubaini kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hiyo unachangiwa zaidi na mila potofu hivyo umetolewa wito kwa watanzania kuungana pamoja katika kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili kwa mtoto wa kike, hususan masuala ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia ambayo bado hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo, hali inayohatarisha mustakabali mzima wa ukuaji wa mtoto kiafya, kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Akizungumza na Wanawake waliokuwa Kliniki katika Zahanati ya Kijiji cha Ikhanoda Wilaya ya Singida mkoani hapa jana, wakati akitoa mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia, kupitia mradi wa ‘Tokomeza Ukeketaji Singida,’ unaofadhiliwa na Ubalozi wa Uholanzi, Afisa Mradi kutoka ESTL, Annamaria Mashaka, alisema ukatili huo unachangiwa zaidi na mila na desturi kandamizi, ambazo zimeegemea zaidi kwenye dhana ya mfumo dume ndani ya jamii.
Mashaka alisema vitendo vya ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ndoa za kulazimishwa imekuwa ni kama mtindo wa maisha kwa baadhi ya wazazi na walezi ndani ya kaya kwa kisingizio cha mila na desturi, hali inayopelekea madhara makubwa katika ukuaji wa (mlengwa) mtoto, ikiwemo kupoteza mwelekeo mzima wa maisha yake na kuathiri maendeleo na utu wake.
Alisema uwepo wa mila na desturi potofu na matokeo hasi ya mfumo dume ni miongoni mwa sababu zinazochagiza kushamiri kwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, huku wazazi na hasa wanaume ndani ya kaya kwa tamaa ya kupata utajiri wa haraka wakijikuta wanawaozesha mabinti zao walio katika umri mdogo, kwa kigezo cha kupatiwa mifugo au mali nyinginezo.
Mashaka alisema mkoa wa Singida bado kuna changamoto kubwa ya idadi ya wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ukatili wa kingono, kimwili, kiuchumi na kisaikolojia. Takwimu za kitafiti zinaonesha kuwa kati ya wanawake 100 ndani ya mkoa huo 31 wamekeketwa, huku wengi miongoni mwao wakijikuta tayari wamefanyiwa ukatili huo katika umri mdogo bila ya wao kujitambua.
Akichukua muda mrefu kufafanua dhana ya Jinsi na Jinsia, sambamba na mila nzuri na mila potofu, ikiwemo uwiano wa majukumu ya mwanaume na mwanamke ndani ya jamii katika muktadha wa dhana ya ukatili wa kijinsia na matokeo hasi ya mfumo dume, Mashaka alisema jamii inapaswa kubadilika, ni wajibu wa kila mtanzania kwa nafasi yake kusimama na kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Aidha, alisema pia ukatili wa kimwili mara kadhaa husababisha majeraha, ulemavu, matatizo ya kisaikolojia na hata vifo kwa akinamama na watoto.
“Ukatili wa kingono mathalani unaleta madhara makubwa katika afya ya mwanamke na mtoto wa kike kwa kusababisha mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa, kuharibu mifumo ya uzazi, Ukimwi,” alisema Mashaka na kuongeza; “Athari hizo ni kikwazo cha maendeleo ya mwanamke na mtoto wa kike katika kupata elimu, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii,” alisema.
Akizungumza na wanafunzi wa shule nne zilizopo Kata ya Ikhanoda za Ikhanoda, Kisisi, Msimii na Sekondari ya Ikhanoda ulipo mradi huo, Mratibu wa mradi huo Edgar Kalugila aliwaeleza athari za ukatili huo wa kijinsia ukiwemo usafirishaji haramu wa binadamu ambapo alihimiza kuunda na kuimarisha Klabu za afya mashuleni.
Aidha Kalugila akizungumzia kushamiri kwa tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu hasa mtoto wa kike, alisema Taifa linapaswa kuwa macho na jambo hilo kwani ugumu, machungu, hasara na mateso wanayoyapata mabinti wadogo wanaokumbwa na kadhia hiyo inasikitisha.
Alisema imekuwa ni kama mtindo wa maisha kwa watoto wa kike wenye umri mdogo kurubuniwa na watu wasiojulikana na kupelekwa kusikojulikana, kwa kigezo cha kwenda kutafutiwa ajira zenye maslahi makubwa, lakini kinyume chake imegeuka kuwa ni janga.
“Niwasihi ninyi wanafunzi msidanganyike na watu hao, kumbuka utakwenda huko kuuzwa, utadhalilika, utatumika kingono, na mwisho wa siku wengi kati ya hao wanaokwenda hurudi wakiwa na majeraha kutokana na mateso na ukatili wa kutisha waliofanyiwa na wengine wakiwa wamepoteza maisha, jambo linaloleta hasara kwa wazazi, ndugu na taifa,” alisema Kalugila.
Kwa upande Mwezeshaji Hawa Hussein kutoka ESTL, alisema kinachosikitisha zaidi ukatili huo na hasa vitendo vya ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni umekuwa ukipelekea madhara ya kiafya katika ukuaji wa mtoto wa kike.
“Mwathirika wa tukio hilo baada ya kufanyiwa ukatili huu hujikuta akikumbwa na kadhia mbalimbali za maradhi, ikiwemo kujifungua mtoto akiwa na tatizo la mtindio wa ubongo,kushindwa kusukuma mtoto wakati wa kujifungua na kupata ugonjwa wa kushindwa kujizuia haja yaani ‘fistula kutokana na baadhi ya mishipa yake sehemu ya uzazi kuathirika’,” alisema Hussein.
Alisema hali hiyo husababishwa na kutokukomaa kwa nyonga za mtoto huyo wa kike, kutokana kuingia kwenye masuala ya uzazi akiwa na umri mdogo hali inayosababisha kushindwa kuhimili baadhi ya vipengele muhimu ikiwemo kusukuma mtoto wakati wa hatua ya kujifungua.