……………………………………………………………
Na Damian Kunambi, Njombe.
Kufuatia uwepo wa tatizo la maji linalowakabili wakazi wa kijiji cha Kiyogo kata ya masasi iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe na kuwalazimu kutumia maji ya mto Luhuhu imepelekea wakazi hao kuliwa na mamba pindi wachotapo maji hayo.
Hayo yameelezwa na wakazi wa kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 667 baada ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuanza ziara yake ya kutembelea wananchi wake wa kata mbalimbali ameanza na kijiji cha Lihagule, Kiyogo na Kingole huku akiwa ameambatana na viongozi wa chama pamoja na wakuu wa idara mbalimbali za serikali.
Wakazi hao wamedai kuwa wamekuwa wakipatwa na misiba mara kwa mara inayosababishwa na mamba hao hivyo wanaiomba serikali iwasaidie kuondoa Mamba hao ili waweze kuchota maji na kufanya shughuli zao za uvuvi kwa uhuru.
Akizungumza kwa uchungu mmoja wa wananchi hao Laurence Mahundi amesema kuwa siku chache zilizopita kuna mwanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi Kiyogo ameliwa na Mamba na matatizo hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hivyo wanaomba serikali iwasaidie.
Alfoncia Haule naye ni mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa wao wakinamama na watoto ndio wanapata tabu zaidi kutokana na tatizo hilo la maji hivyo wameiomba serikali kupitia mbunge wao kuwasaidia kupata pampu ya maji itakayokuwa inavuta maji mtoni na kuleta shuleni ili wanafunzi wasiendelee kwenda mtoni.
“Tunaiomba serikali ituangalie kwa jicho la kipekee kwani sisi huku tumekaa kama tupo kisiwani maana tumekuwa tukiwekwa nyuma katika kuletewa maendeleo hivyo kwenye suala hili la maji tunafahamu ni tatizo la kwa kata yote hii ya masasi ila tunaomba kwa sisi wa Kiyogo tupewe kipaumbele maana tunateketea! Mamba wanatutesa sana!”, Alisema Bi. Haule.
Sanjari na tatizo hilo la maji kwa wakazi hao pia tatizo hilo limeonekana kuwepo katika kata nzima ya masasi pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara inayotoka Lihagule na Kingole kuelekea kijijini hapo kwani wamekuwa wakishindwa kusafirishia mazao yao ya biashara kama korosho, Mahindi pamoja na mihogo kutokana na ubovu huo wa barabara unaopelekea vyombo vya moto kutokufika maeneo hayo sambamba na changamoto ya umeme.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga aliwafuta machozi wananchi hao kwa kuwapa taarifa njema juu ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.
Amesema suala hilo tayari alianza kulifanyia kazi muda mrefu kwa kuliwasilisha wizara husika ambapo alikutana na waziri wa maji Juma aweso wakiwa na naibu waziri wake Meryprisca Mahundi pamoja katibu mkuu wote kwa pamoja walilipokea jambo hilo ambapo waziri huyo alimuagiza katibu mkuu kutenga kiasi cha shilingi Milioni 268 katika kipindi hiki cha mwezi julai ili kutatua tatizo hilo kwa wananchi.
“Suala la maji halina mbadala wowote ambao unaweza kubadili na ndiomaana pamoja na wananchi kuliwa na mamba lakini bado mnaenda mtoni kuchota maji hayo kwakuwa hamna njia nyingine mnayoweza kutumia kupata maji. Ili niweze kuokoa maisha ya wananchi wangu niliona nipambane mpate maji na suala hilo linaelekea kufanikiwa”, Alisema Kamonga.
Ameongeza kuwa fedha hizo za mradi wa maji atahakikisha anazifuatilia kwa ukaribu ili zisiweze kupotea hata shilingi bali fedha zote zitumike katika mradi huo.
Aidha kwa upande mwenyekiti wa CCM wilayani humo Stanley Kolimba pamoja na katibu wa chama hicho Bakari Mfaume wamempongeza mbunge huyo kwa kutimiza vyema wajibu wake pamoja na ilani ya chama hicho kwani mbunge huyo amekuwa akiwatembelea na kusikiliza kero za wananchi wa jimboni kwake kitu ambacho kimekuwa kikileta matokeo mazuri katika uongozi wake.
Pia wamewaomba wananchi hao kuonyesha ushirikiano wa kutosha kwa mbunge huyo ili aweze kupata nguvu zaidi katika kuleta maendeleo.