Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akizungumza na watendaji wa kada ya Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani na Manunuzi kutoka katika Taasisi zake katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Chimwaga jijini Dodoma.
Watendaji wa kada ya Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani na Manunuzi kutoka katika Taasisi zilizo chini ya Wizara wakimsikiliza Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Chimwaga jijini Dodoma ambapo Waziri Aweso ametaka watendaji hao kwenda kufanya kazi kwa weledi na nidhamu ya matumizi ya fedha za maji.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiwa na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa kada ya Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani na Manunuzi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Chimwaga jijini Dodoma.
*********************
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka watendaji wa kada ya Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani na Manunuzi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zinazoelekezwa katika kutekeleza miradi ya maji.
Waziri Aweso amesema hayo leo katika kikao kazi kilichowakutanisha kwa mara ya kwanza Watendaji wa kada hizo katika Ukumbi mdogo wa Chimwaga jijini Dodoma.
Amesema Wizara imeajiri wataalamu wa kada hiyo wenye uwezo mkubwa ambao anaamini kwa kushirikiana kwa pamoja wataweza kukwamua changamoto za miradi ya maji hasa katika upande wa manunuzi na ulipaji wa wakandarasi kwa wakati.
“Ninyi ndio wapishi wa miradi nendeni mkatafute wakandarasi wazuri wenye sifa, watakaoweza kutekeleza miradi kwa wakati na mkandarasi asiyekuwa na uwezo asipewe kazi na wala msitoe kazi kwa kupeana,” Amesema Waziri Aweso.
Ameongea kuwa wakandarasi wote ambao wameichafua Wizara ya Maji wasipewe kazi ili wakandarasi wenye sifa na uwezo waweze kupata kazi hizo na kutekeleza miradi ya maji kwa kasi inayotakiwa na kiwango kinachokubalika.
Ameongeza, viongozi wa Wizara hawatakuwa tayari kuona mtumishi yeyote anakuwa kikwazo kwa kutofuata taratibu na kanuni zilizowekwa katika kutekeleza majukumu na mwenye kufanya hivyo uongozi hauta sita kuchukua hatua za kinidhamu.
Aidha, Waziri Aweso amemsimamisha kazi Afisa Ugavi Bw. Victor Kaphipa ambaye kwa sasa kituo chake cha kazi ni Bonde la Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma kutokana na madai ya kuwa dalali ndani ya Wizara na kuchafua taswira ya Wizara.
Amesema Wizara haina mashamba wala viwanja hivyo, hakuna haja ya kuwa na watumishi ambao ni madalali wa Wakandarasi na watoa huduma wanaoomba kazi katika Wizara.
Waziri Aweso amesisitiza kwamba watumishi wote katika sekta ya maji kufanya kazi kwa uadillifu, ushirikiano na umakini wa hali ya juu ili kuongeza kasi ya kutekeleza miradi ya maji na kuweza kumpatia mwananchi majisafi na salama na yenye kutosheleza kwa wakati.