Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Na Mazingira Mhe. Selemani Jafo (aliyenyanyua mikono), akiongea na Msimamizi Mkuu wa kiwanda cha Lake Cement Limited Bw. Biswajeet Malkin(kulia) wakati wa ukaguzi katika kiwanda hiko, Kilichopo Kimbiji Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Na Mazingira Mhe. Selemani Jafo (aliyenyanyua mkono), akitoa maelekezo kwa Msimamizi wa kiwanda cha Tanzania Raidar Company Limited Bi. Ping Zhang kinachozalisha bomba na chupa za plastiki kutokana na taka za plastiki kilichopo Kisarawe II Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa akielezea jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Selemani Jafo katika kiwanda cha kuzalisha mafuta machafu kwa kutumia matairi chakavu kilichopo kisarawe II jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya majitaka yanayozalishwa kiwanda cha Raidar na kwenda kwenyemakazi ya watu.
****************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Mkamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, ametoa miezi mitatu kwa kiwanda cha Tanzania Raidar Company Limited kubadilisha mfumo wa maji taka. Ameyasema hayo alipotembelea kiwanda hicho kilichopo maeneo ya Kisarawe II Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam.
Mhe. Jafo ametembelea kiwanda cha Raidar kinacho jishughulisha na urejerezaji wa taka za plastiki kuwa bidhaa aina ya mabomba na chupa za plastiki. Akiwa katika ziara hiyo amebaini utiririshwaji wa maji machafu kutoka kiwandani hapo kwenda katika makazi ya watu na kupelekea uchafuzi wa mazingira na malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokaa karibu na kiwanda hicho.
“Nimefurahishwa na kiwanda hiki kurejereza taka kwani inasaidia kutoa taka zinazozagaa mtaani, hii ni njia nzuri ya utunzaji wa mazingira, lakini kitendo cha kutiririshaji wa maji machafu kutoka kiwandani na kwenda kwenye makazi ya watu sio suala zuri kiafya na kimazingira. Hivyo natoa miezi mitatu kuhakikisha tatizo hilo linashughulikiwa na sitaki kusikia malalamiko tena” Mhe. Jafo
Vile vile Mhe. Jafo ametembelea kiwanda cha Gueng Cheng Industry Limited kilichopo Kisarawe II Wilaya ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam, kiwanda kinachozalisha mafuta machafu yanayotokana na matairi yaliyotumika. Mhe. Jafo Amesema kuwa kiwanda hiki kinalalamikiwa na wananchi kutokana na moshi mwingi na vumbi linalotokana na uchomaji wa matairi kiwandani hapo.
“Sijaridhika kabisa na utendaji wa kazi katika kiwanda hiki, natoa miezi sita kuhakikisha mitambo inayotumika ibadilishwe ili kuzuia moshi unaokwenda kwenye makazi ya watu ambao unaathari kubwa kiafya kwa wananchi pamoja na mazingira. Pamoja na hayo kiwanda hiki kipo katika makazi ya watu hivyo ni bora kutafuta eneo lingine ili isiwe usumbufu kwa wakazi hao. Pia naiagiza NEMC kufatilia hili na baada ya miezi sita nitarudi kuangalia utekelezaji” Mhe. Jafo
Kwa upande wake meneja wa NEMC Mashariki Kusini Bw. Hamad Taimuri, amesema kuwa amepokea maelekezo ya Mhe. Waziri Jafo na ufuatiliaji wa viwanda vyote viwili utafanyika ili kuhakikisha wanafanya uzalishaji wao bila ya kuathiri mazingira na Afya kwa watu. Ameendelea kusema kuwa ni kweli wamepata malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya uchafuzi wa mazingira kutoka katika viwanda hivyo na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Mkazi wa Kisarawe II Bw. Said Bomeza, ameiomba Serikali kufuatilia suala hili kwani wananchi wanateseka sana na wawekezaji wasiozingatia sheria. Ameendelea kusema kuwa japo kiwanda kinachotoa moshi wamepewa miezi sita lakini Maisha ya watu yako hatarini hivyo ingekuwa bora baada ya miezi sita kufatilia hilo na kukiwajibisha kiwanda hicho.
Waziri Jafo pia ametembelea kiwanda cha Lake Cement Limited kiwanda cha kuzalisha saruji kilichopo Kimbiji Wilaya ya Kigamoni jijini Dar es Salaam, kujionea namna wanavyofanya uzarishaji wake bila ya kuathiri mazingira na afya kwa watu. Mhe. Jafo amekipongeza kiwanda hicho kwa wanavyotunza mazingira na amewataka wazarishaji wengine wa saruji kuiga mfano wa tekinolojia wanayotumia ambayo haichafui mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa, amesema kuwa Wilaya ya kigamboni inauwekezaji wa viwanda hivyo kama ofisi ya wilaya kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigamboni itaendelea kukagua viwanda hivyo ili kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji wenye tija kwa maslahi ya Taifa.