Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Mbaraka Stambuli akifungua kongamano la kujadili mifumo ya chakula kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini leo mjini Njombe.
Kinara wa Mifumo ya Chakula (National Food System Champion) na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Neema Lugangira akizungumza kwenye kongamano la mifumo Nyanda za Juu Kusini leo mjini Njombe ambapo ametoa wito kwa wadau kuangalia mabadiliko ya tamaduni ili kuwa na lishe bora nchini.
Mwakilishi wa mratibu wa Mifumo ya Chakula toka Wizara ya Kilimo Bi. Magret Natai akizungumzia lengo la kongamano hilo ambapo amesema Tanzania inautoshelevu wa chakula wa asilimia 126 lakini bado kuna tatizo la udumavu hivyo kuhitaji mjadala wa kukuza uelewa juu ya lishe bora.
Mwakilishi wa kikundi cha Wakulima wa Parachichi Ruvuma Bw. Beno Mgaya akizungumzia umuhimu wa matunda kwenye kuboresha mifumo ya chakula nchini.
Picha ya pamoja ya wajumbe toka mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma,Mbeya na Songwe wanaoshiriki kongamano la kujadili mifumo ya chakula linaloratibiwa na Wizara ya Kilimo leo mjini Njombe kwa lengo la kujadili changamoto za mifumo ya chakula na lishe.
(Habari na Picha Wizara ya Kilimo)
*************************
Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau inaendesha makongamano kuhusu mifumo ya chakula kwa lengo la kukusanya maoni yatakayosaidia nchi kuboresha mifumo ya chakula na kuimarisha lishe ikiwa ni utekelezaji wa malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
Akifungua kongamano la mifumo ya chakula kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini leo (01.07.2021) mjini Njombe kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Mkurugenzi Msaidizi Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mbaraka Stambuli, alisema mikoa ya Njombe ,Songwe, Ruvuma na Rukwa inaongoza kwa kuwa na watoto wenye udumavu .
Aliongeza kusema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndio inaongoza kwa kwa uzalishaji mkubwa wa chakula lakini jambo la kushangaza ukanda huu ndio wenye hali duni ya za lishe.
Stambuli alisema kongamano la mifumo ya chakula linalenga kujadili changamoto muhimu katika mifumo ya chakula kwa kuzingatia ikolojia kwenye kanda ili kufanya dunia kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora.
“Kwa mfano mkoa wa Njombe ndiyo wenye asilimia kubwa ya Watoto wenye udumavu (53.6%) amba[o mikoa mingine yenye udumavu zaidi ya asilimia 40 ni Songwe (43.3%), Ruvuma (41.0%), Rukwa ( 47.9 %) na Iringa (47.1%) ambapo takwimu hizi zinaashiria matatizo katika mfumo wa chakula hivyo wadau wanatakiwa kutafuta majawabu kuboresha hali ua lishe nchini “ alisema Stambuli.
Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu Mifugo alibainisha kuwa mfumo wa chakula una mafungamano na changamoto ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi pia mwenendo mbaya wa hali ya hewa, magonjwa sugu, maonjwa yasiyo ya kuambukiza na lishe duni ikiwemo athari za kutozingatiwa u salama na ustawi wa wanyama.
Stambuli alibainisha kuwa Wizara ya Kilimo imepewa jukumu la kuratibu na kuhakikisha wadau wote wa sekta ya umma na binafsi katika mfumo wa chakula wanashiriki mijadala ambapo mapendekezo ya nchi yatawalishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu New York Marekani.
Akizungumza kuhusu lengo la kongamano la mfumo ya chakula Mwakilishi toka Wizara ya Kilimo Magret Natai alisema maana ya ‘ Mfumo wa Chakula ni mkusanyiko wa shughuli zinazohusiana na uzalishaji ,usindikaji,usafirishaji ,uhifadhi na ulaji wa chakula ‘.
Natai alibainisha kuwa kupitia kongamno hilo wadau watapata muda wa kujadiliana mifumo sahihi itakayoongeza kasi ya namna dunia inavyozalisha, inavyotumia chakula na mtazamo wake kuhusu chakula.
Wakizungumza kwenye kikao hicho wawalikishi wa wakulima kutoka Njombe,Iringa,Mbeya ,Songwe na Ruvuma wakiwemo Benno Mgaya kutoka SAGCOT Songea alisema ili kukabiliana na changamoto za udumavu elimu kwa shule za msingi na sekondari ni muhimu ikiwemo suala la lishe bora.
“Ni muhimu shule zote nchini ziwe na bustani za mboga mboga na matunda ili kuwajengea watoto uelewa wa umuhimu wa lishe bora wakiwa bado wadogo” alisisitiza Mgaya
Naye Martin Haule mfugaji kutoka wilaya ya Njombe alisema Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alisisitiza suala la lishe bora ili kuepukana na hali ya udumavu ambapo amewataka wazazi kutoa chakula bora na kwa wakati kwa watoto wao .
Haule alibainisha kuwa kwa Njombe tatizo la udumavu linachangiwa na “ wazazi kwenda mashambani na kurudi jioni hivyo watoto wanashinda na njaa au watoto wanapewa ulanzi na komoni badala ya chakula bora hivyo udumavu kuendelea” alisema.
Majadiliano kuhusu mifumo ya chakula yanafanyika nchini kwenye kanda mbalimbali chini ya uratibu wa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Dkt. Honest Kessy (Country Converner) aliyeteuliwa kuratibu mijadala hii kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Andrew Massawe.
Kongamano la Mifumo ya Chakula Nyanda za Juu Kusini Njombe linafanyika sambamba na jingine linalofanyika Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza ili kupata mapendekezo ya nchi na hatua za kuimarisha mifumo ya chakula yakihusisha wadau wa maendeleo wakiwemo AGRA, FAO, WFP, GAIN na SAGCOT.