Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Omar Dadi Shajak akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya kitaifa ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, wanawake na watoto Zanzibar walipokutana Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Mjini Unguja.
Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambae ni Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji Zanzibar Haroun Ali Suleiman akifungua Mkutano wa kamati hiyo kujadili mambo mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, wanawake na watoto Zanzibar wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wa kikao hicho iliyotolewa na Waziri Haroun Ali Suleiman (hayupo pichani).
Picha na Makame Mshenga.
************************
Na Issa Mzee Maelezo 30/06/2021
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema umefika wakati wa kila mmoja kuwajibika ipasavyo ili kutokomeza vitendo vya udhalilishaji nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Waziri Haroun amesema tatizo la udhalilishaji linaendelea kukemewa vikali na Serikali pamoja na wadau mbalimbali hivyo nguvu ya pamoja inahitajika ili kutokomeza tatizo hilo.
Alisema lengo la kikao hicho kilichoshirikisha wadau mbalimbali wa udhalilishaji ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama ni kukusanya maoni ya wadau ambayo yatasaidia kupanga mikakati madhubuti ya kupambana na udhalilishaji nchini.
Alieleza kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto ni miongoni mwa vitendo viovu ambavyo hudumaza ustawi wa jamii na maendeleo ya watoto wengi nchini.
“Hivi sasa tunataka tumalize kabisa vitendo hivi ili iwe ni historia kwa Zanzibar visiwepo tena vimetutosha watoto wetu bado wanadhalilishwa sasa udhalilishaji basi”, alisema Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo alipongeza Serikali kwa kuanzisha mahakama ya udhalilishaji ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza jitihada za kumaliza udhalilishaji nchini.